• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China: Uhifadhi mazingira Afrika moja ya vipaumbele vyetu

    (GMT+08:00) 2018-05-30 12:42:40

    Na Majaliwa Oswero

    WIZARA ya Ekolojia na Mazingira ya serikali ya China imesema inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha mazingira ya bara la Afrika yanalindwa dhidi ya uchafuzi, athari ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto mbalinmbali zinazotokana na uharibifu wa mazingira.

    Bara la Afrika kwa sasa linapambana kufa na kupona kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali zinazotokana na uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na ukataji ovyo miti, mmomonyoko wa ardhi, mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla na uharibifu wa uoto wa asili unaosababisha vyanzo vya maji kukakuka.

    Uhifadhi wa mazingira, maisha ardhi, maisha maji na tabianchi ni baadhi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 17 ambayo dunia imejiwekea kufanikisha kufikia mwaka 2030.

    Akizungumza na waandishi wa habari kutoka barani Afrika walio katika programu maalum ya mafunzo jijini Beijing, Meneja wa Programu ya Ushirikiano wa Uhifadhi wa Mazingira, Kitengo cha Asia na Pacific kutoka wizara ya Mazingira na Ekolojia, Bi. Lu Diyin, alisema utunzaji wa mazingira ni moja ya maeneo ambayo serikali ya China inayapa kipaumbele.

    Alisema ili kuhakikisha ushirikiano huo unapata uzito unaostahili, Kituo cha Ushirikiano wa Uhifadhi wa Mazingira kati ya China na Afrika kinategemewa kuzinduliwa mwezi wa tisa katika mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, FOCAC.

    Bi Lu alisema kati ya mwaka 2005 na 2015, kitengo cha Ushirikiano cha Utunzaji wa Mazingira umefanikiwa kuandaa warsha 45 na kutoa mafunzo maalum juu ya namna bora ya uhifadhi wa mazingira kwa maafisa zaidi ya 1,500 kutoka nchi za bara la Afrika.

    Mafunzo yaliyotolea ni pamoja na uhifadhi wa vyanzo vya maji dhidi ya uchafuzi na uharibifu, ekolojia, utunzaji wa mazingira na menejimenti ya mazingira maeneo ya mijini.

    Alisema pia kuwa wizara imetekeleza maazimio ya Johannesburg yaliyofikiwa katika mkutano wa FOCAC, mwaka 2015 nchini Afrika Kusini juu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira ambayo pamoja na mambo mengine, yalihimiza 'uwekezaji wa kijani' barani Afrika.

    Bi.Lu alisema kuanzishwa kwa kituo cha Ushirikiano cha Uhifadhi wa Mazingira kati ya China na Afrika kutasaidia kubadilishana mbinu za kiteknolojia na taarifa muhimu za namna bora ya kutunza mazingira na kulinda uoto asili kati ya pande hizo mbili.

    Aliongeza pia kuwa wanafanya kila lililo ndani ya uwezo wao kuhaikiksha uwekezaji wao barani Afrika hauleti uharibifu wa mazingira.

    Hivi karibuni, akizungumza na waandishi wa habari kutoka barani Afrika, Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Dai Bing alisema kwamba China inachukua tahadhari kubwa kuhakikisha shughuli zake barani Afrika haziichangii katika uchafuzi wa mazingira.

    "Tunachukua tahadhari na hatua stahiki kuhakikisha hatuleti uchafuzi wa mazingira barani Afrika. hatuna nia wala mpango wa kuchafua anga za bluu za Afrika, milima mizuri wala maji safi yaliyopo barani humo," alisisitiza.

    Mkurugenzi huyo aliendelea kueleza kuwa miaka 20 iliyopita, serikali ya China iliweka wazi kuwa haitaki kufata mfumo wa mataifa mengine yaliyoendelea ambayo huchafua mazingira kwanza na baadae kuanza kushugulikia namna ya kutatua.

    Bw. Dai alitolea mfano jiji la Beijing, kwa kusema kuwa miaka saba iliyopita jiji hilo ambalo ni mji mkuu wa China ulighubikwa na uchafuzi wa hewa kwa kiasi kikubwa.

    Kutokana na hali hiyo, Bw. Dai alisema limekuwa funzo kubwa sana kwao na sasa wanachukua hatua stahiki kabla, kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo popote pale wanapoendesha shughuli zao za uzalishaji.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako