• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China kuendelea kushirikiana na Afrika kuboresha afya

    (GMT+08:00) 2018-06-05 15:16:44

    China imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na Afrika katika sekta ya afya kwa kutoa misaada ya kitaalamu na kuboresha miradi inayotekelezwa kwa pamoja kati yake na nchi za bara hilo.

    Imeeleza itaendelea kutuma timu ya wataalamu wa afya, kutoa ushauri wa kitaalamu na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya afya ya uzazi na mtoto na vita dhidi ya malaria.

    Hayo yameelezwa jana na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Tume ya Taifa ya Afya, Bw. Feng Yong, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka Afrika waliotembelea ofisi za tume hiyo jijini Beijing.

    "Sekta ya afya ni moja ya maeneo muhimu tunayoshirikiana na bara la Afrika. Tunatoa misaada ya kitaalamu, kufadhili miradi mbalimbali na pia kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa watoa huduma za afya kutoka nchi mbalimbali za Afrika," alisema Bw. Feng Yong.

    Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo, hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu 2018, jumla ya wataalamu 953 kutoka China walikuwa katika bara la Afrika wakitoa huduma za afya katika nchi za Afrika 40.

    Bw. Feng Yong alisema kuwa ushirikiano kati ya China na bara la Afrika katika sekta ya afya ulianza mwaka 1963 na kuwa wameweza kutuma timu ya wataalamu kwenda barani humo takribani 20,000.

    "Tumekuwa pia tukitekeleza miradi mbalimbali ya afya kwa kushirikiana na hospitali mbalimbali kutoka nchi za Afrika, lengo kubwa ni kubadilishana utaalamu, uzoefu na pia kupiga hatua ya pamoja katika maendeleo ya sekta ya afya." aliongeza Bw. Feng Yong.

    Alieleza kuwa China hadi sasa ina ushirikiano wa pamoja na hospitali 15 kutoka nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, Zimbabwe, Zambia, Gambia, Mali Feng Yong alisema kuwa China pia imekuwa ikishirikiana na Afrika katika mapambano dhidi ya malaria, ugonjwa ambao huua idadi kubwa sana ya watu barani humo.

    Hadi kufikia mwaka jana, kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ugonjwa wa malaria umeisha kabisa nchini China na kwa sasa katika ushirikiano wao na Afrika wanajaribu kubadilishana njia mbalimbali za kitaalamu iliyofanya nchi iyo yenye idadi kubwa ya watu duniani kutokomeza malaria.

    Bw. Feng Yong aliongeza kuwa mwaka jana 2017, watumishi wa sekta ya afya zaidi ya 1,000 kutoka barani Afrika walipewa mafunzo mbalimbali nchini China.

    China na Afrika pia kwa mujibu wa Bw. Feng Yong zinashirikiana katika usafirishaji na uuzaji wa vifaa tiba na dawa, akibainisha kuwa mwaka 2015, biashara ya dawa na vifaa tiba kati ya pande hizo mbili zilifikia zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 2.4.

    Naibu Mkurugenzi huyo pia aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Agosti 17 hadi 20 mwaka huu jijini Beijing, kutakuwa na mkutano maalum kati wataalamu wa sekta ya afya kutoka Afrika na China kujadili mambo mbalimbali juu ya maendeleo na ushirikiano wa sekta hiyo.

    "Huu mkutano utafanyika siku chache kabla ya mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, FOCAC, utakaofanyika mwezi Septemba. Mapendekezo juu ya namna bora ya kuboresha sekta ya afya yatapelekwa katika mkutano wa FOCAC kwa hatua zaidi." alisema Bw. Feng Yong.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako