Oswero, Bijie
Wawakilishi kutoka Afrika katika mkutano wa Ushirikiano wa China na Afrika katika kupunguza umaskini wameshauri nchi zao kuiga mfano wa China katika vita dhidi ya umaskini.
Wamesema China imefanikiwa kupambana na umaskini kwa kuwa na sera madhubuti, mipango mizuri katika sekta ya kilimo na uwezeshwaji ambayo ni chachu ya kupambana na umaskini.
Mkutano kati ya Afrika na China juu ya kupunguza umaskini umefanyika wiki chache kabla ya mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na China, FOCAC, unaotegemewa kufanyika mapema mwezi ujao.
Viongozi mbalimbali kutoka Afrika baada ya mkutano uliofanyika jijini Beijing uliojikita katika kujadili njia mbalimbali za ushirikiano baina ya pande hizo mbili katika kupunguza umaskini, walitembelea mji wa Bijie, jimboni Guizhou na kujionea jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya China kutatua changamoto ya umaskini kwa wananchi wake.
Guizhou ni jimbo ambalo wakazi wake kwa miaka mingi walikuwa wanaishi katika wimbi kubwa la umaskini, lakini baada ya serikali kuanzisha programu mbalimbali za kupambana na janga hili, wananchi wake sasa wameweza kuondokana na tatizo la umaskini.
Viongozi hao kutoka Afrika walishauri serikali zao kuiga mfano wa China katika vita dhidi ya umaskini kwa kuwa na mipango ya kueleweka, mikakati sahihi ya utekelezaji wa mipango hiyo pamoja na kuweka wazi namna bora ya ufadhili wa mipango hiyo.
Mwakilishi kutoka Tanzania ambae ni Katibu Tawala, Mkoa wa Morogoro, Bw. Clifford Tandari aliipongeza China kwa hatua nzuri ya mapambano dhidi ya umaskini ambayo imechangiwa na uwezeshwaji wa serikali kwa wananchi wake.
Alisema pamoja na kuwa serikali za Afrika zimekuwa zikijitahidi kuchukua hatua mbalimbali kupiga vita umaskini, jitihada zaidi zinahitajika hasa katika kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, ambayo huajiri zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wote barani humo.
Alisema serikali za Afrika hazina budi kuhakikisha zinaweka mkazo mkubwa katika teknolojia na uimarishaji wa miundombinu muhimu katika kuinua sekta ya kilimo.
Waziri wa Kilimo wa zamani wa Uganda ambae pia alikuwa mwakilishi wa shirika la Chakula na Kilimo duniani, FAO, Bi. Ms Victoria Sekitoleko alisema serikali za Afrika lazima ziige mfano wa China kwa kuboresha kilimo kama zina nia ya dhati katika kupambana na umaskini.
Alisema kuwa wakulima lazima wapatiwe zana husika za kilimo zikiwemo pembejeo ambayo ni pamoja na mbolea, madawa na pia kuhakikisha kunakuwa na soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa kuna mambo mengi Afrika inatakiwa kujifunza kutoka China ikiwemo kuanzisha ukanda maalumu kwa ajili ya viwanda ambao utachangia kuajiri watu wengi pamoja na kutengeneza soko imara kwa ajili ya mazao yanayozalishwa na wakulima.
Bi. Sekitoleko alisema hatua ya China kuanzisha miradi mbalimbali kama kilimo cha mboga, matunda na ufugaji wa ng'ombe ambayo humilikiwa kwa pamoja na kaya maskini inasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya umasikini wa kipato.
Alishauri serikali za bara la Afrika kuiga mfano huo ambao umesaidia kwa kiwango kikubwa sana kuondoa asilimia kubwa ya wakazi wa China katika dimbwi la umaskini.
Kamishna wa Umoja wa Afrika anaeshughulikia masuala ya kilimo na uchumi vijijini, Bi. Josefa Leonel Correia Sacko alisema pamoja na uchumi wa Afrika kuonekana kukua, umaskini bado ni janga linalohitaji hatua za haraka na za kudumu kutatua.
"Ukosefu wa teknolojia ya kisasa ni moja kati ya sababu zinazochangia umaskini kushamiri barani Afrika. tunahitaji mapinduzi ya teknolojia katika sekta ya kilimo. Tunatakiwa pia kushirikiana kwa karibu na China kwenye hili lakini pia kushirikisha sekta binafsi," aliongeza.
Alisema inasikitisha kuona Afrika pamoja na kuwa na ardhi ya kutosha yenye rutuba kwa ajili ya kilimo pamoja na nguvu kazi ya kutosha, bara hili bado linapata mavuno hafifu na duni.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |