• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yashauri namna bora ya kupambana na umaskini

    (GMT+08:00) 2018-08-20 09:11:17

    Oswero, Beijing

    China imependekeza uimarishwaji wa tafiti, uendelezwaji wa vipaji kwa vijana na uanzishwaji wa miradi ya mifano kati yake na Afrika ili kufanikiwa katika vita dhidi ya umaskini.

    Imesisitiza kuwa vita dhidi ya umaskini na upatikanaji wa maendeleo endelevu ni agenda ya pamoja kati ya Waafrika na Wachina, hivyo pande hizo mbili hazina budi kushirikiana katika kubadilishana uzoefu, mawazo na fikra juu ya namna bora ya kupunguza na kumaliza kabisa umaskini.

    Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa ofisi ya kupambana na umaskini ya baraza la serikali ya China Bw. Liu Yongfu jijini Beijing akihutubia wawakilishi kutoka nchi mbalimbali za Afrika waliokutana hapa katika mkutano wa kupambana na umasikini kati ya China na Afrika.

    Alisema ili kufikia agenda ya UN 2030 ya maendeleo endelevu, China na nchi zinazoendelea ikiwemo bara la Afrika lazima ziweke malengo yanayotekelezeka ya namna ya bora ya kuondokana na umaskini.

    "China iko tayari kushirikiana na nchi zote za Afrika katika hii vita dhidi ya umaskini kwa kubadilishana uzoefu, kuimarisha tafiti na ubunifu pamoja na kusaidiana kwa namna yoyote ile ili kupata matokeo chanya," alisema Bw.Liu.

    Alisema Afrika ina nguvu kazi ya kutosha ambayo asilimia kubwa yake ni vijana huku ikikadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2025 itakuwa na vijana wa umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 wapatao milioni 200, kundi ambalo ni muhimu katika kuleta mabadiliko.

    Bw. Liu alisema katika mkutano wa FOCAC unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao, agenda za Ukanda Mmoja, Njia Moja, Mpango wa Maendeleo Endelevu wa UN 2030 pamoja na Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, zitajadiliwa kwa pamoja, zikiwa ni miongoni ya mikakati yenye malengo sawa --kupambana na kutokomeza umaskini.

    Aliongeza kuwa Afrika siyo tu ni sehemu ya Ukanda Mmoja, Njia Moja lakin ni wahusika wakuu katika mradi huo wa mabilioni ya dola za Kimarekani ambayo unawiana kabisa na utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali chini ya Agenda 2063 ya AU.

    "Ukanda Mmoja, Njia Moja inatazamiwa kuleta msukumo wa kipekee katika harakati ya mapinduzi ya viwanda barani Afrika, uendelezwaji wa miji na majiji, ukuzaji wa shuguli za kilimo na kuleta fursa mbalimbali yenye tija katika vita dhidi ya umaskini kati ya China na Afrika," aliongeza Bw. Liu.

    Alieleza kuwa Afrika ina mengi ya kujifunza kutoka China hasa katika vita dhidi ya umaskini kwani miaka michache iliyopita ilikuwa moja kati ya nchi zilizokuwa na uchumi usiyoridhisha huku wananchi wake wakiishi katika umaskini.

    Kutokana na juhudi mbalimbali chini ya viongozi wake, Bw. Liu alisema kuwa China imeweza kutekeleza mipango na miradi mbalimbali ambayo imeiwezesha sasa kuwa nchi ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani.

    Aliongeza kuwa pamoja na jitihada hizo bado wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha takribani milioni 30 ya Wachina ambao bado wanaishi katika umaskini wanakwamulia na kuwezeshwa kuishi maishi mazuri.

    Bw. Liu pia alisema ushirikiano katika kubadilishana uzoefu juu ya mbinu bora ya kupambana na umaskini kati ya China na Afrika ulianza mwaka 2015 na hadi sasa mikutano tisa imefanyika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako