• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Chama tawala nchini Kenya kimetangaza nia ya kufuata nyayo za Chama cha Kikomunisti cha China

    (GMT+08:00) 2018-10-22 08:46:43

    Na Eric Biegon - NAIROBI

    Chama cha Jubilee cha Kenya kimeanza mchakato wa kuratibu mfumo na sera zake na kuweka msingi imara wa kisiasa. Wakati ambapo mahusiano baina Nairobi na Beijing yanaendelea kumawiri, viongozi wa chama hicho tawala nchini Kenya wameweka wazi nia yao ya kufuata nyayo za Chama cha Kikomunisti cha China huu ukiashiria sura mpya ya ushirikiano wa kisiasa.

    Akizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Katibu Mkuu wa chama hicho Raphael Tuju alisema nchi hiyo ya Afrika Mashariki ina mengi ya kujifunza kutokana na jinsi chama cha kikomunisti kimeendeleza mambo yake hasa kwa kuelekeza nchi katika njia ya mafanikio. Alisema chama hicho kinataka kujifunza mbinu bora ya kuendesha mambo yake kwa manufaa ya raia.

    Kwa mujibu wa Tuju ambaye pia ni waziri katika serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, Kenya iko tayari kupata masomo kutoka CPC kuhusu jinsi ya kuimarisha chama hicho cha kisiasa pamoja na kukuza uchumi na kufikia maendeleo endelevu.

    "Mwaka 1961, Pato la taifa la Kenya kwa kila mtu ilikuwa mara nne zaidi ilipolinganishwa na China. Lakini kwa sasa pato hilo ni dola za Marekani 1,450 katika Kenya ikilinganishwa na dola za Marekani 8,875 katika China. Pato la taifa la China limepanda zaidi ya mara 50, ilihali katika Kenya, limepanda kwa mara tatu tu. Tunapaswa kufahamu mkondo uliochukuliwa na China katika kipindi cha miaka 40 iliyopita," Alisema Tuju.

    Tuju, ambaye pia nj msemaji wa chama cha Jubilee, aliweka wazi kuwa chama hicho tawala inataka kupata ufahamu zaidi kuhusu muundo wa chama cha CPC ambacho kina miaka 97 tangu kuanzishwa kwake.

    Kwa maoni yake kuanzishwa kwa shule ya chama cha CPC kimenufaisha uongozi wa chama hicho ambao pia umetekeleza jukumu muhimu katika mageuzi nchini China kwa miaka mingi.

    Kulingana na Tuju, msingi wa utulivu wa nchi hiyo uliwekwa na chama cha CPC baada ya utawala uliojaa mzozano kabla ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949.

    "Ni wazi kote duniani kwamba wakati chama tawala cha siasa ni imara na thabiti, nchi pia inakuwa imara. Ushindani wa kisiasa unazua mzozano na iwapo chama kitashindwa kuimudu basi mzozano huo utaenea nje ya chama. Kwa mara nyingi hii inasababisha ubishi baina ya jamii kwani vyama vyetu vya kisiasa vina asili ya kikabila." alisema.

    Tuju anakiri kwamba Jubilee imependezwa na wazo la chuo cha chama kama ilivyoanzishwa na CPC. Kwa jinsi ambavyo CPC imekuza uwanachama wake kufikia milioni 90, msemaji huyo anasema Jubilee itatumia shule ya chama kushirikiana na Wakenya na pia kujenga uwanachama wake kuambatana na itikadi, sera na programu zake.

    Anasema hii ndio njia ya pekee ya kujenga chama kinyume na hali ya sasa ambapo vyama vingi vinahamasishwa kwa misingi ya kikabila.

    "Tumegundua kuwa kama chama cha Jubilee, tuna deni kwa vizazi vijavyo la kuleta udhabiti wa siasa za chama na taifa hili. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kuinua nchi hii kufikia ngazi ya juu." alisema.

    Maneno yake yaliungwa mkono na Li Xuhang, ambaye ni mshauri katika ubalozi wa China nchini Kenya. Li alielezea umuhimu wa Kenya kuwa na utulivu wa kisiasa ili kuvutia wawekezaji wa kigeni, kuendeleza miundombinu pamoja na kukuza uchumi wake.

    Bwana Li alisema shule ya chama cha CPC kimekuwa na jukumu kubwa la kuchochea ukuaji wa chama hicho kutoka idadi ndogo ya wanachama 23 hadi wanachama karibu na milioni 90 kwa sasa.

    "Ili kukuza chama cha kisiasa, kuna haja ya kuunganisha mawazo na kisha kuchukua hatua, na CPC iliweza kuafikia hilo kupitia kwa shule ya Chama," alisema.

    Katika vita dhidi ya ufisadi, Tuju anasema Kenya ina mengi ya kujifunza kutoka Beijing, huku akigusia jinsi utawala wa rais Xi umefanikisha vita dhidi ya rushwa kote nchini China. Anasema mfumo unaotekelezwa na China kupigana na ufisadi umezuia kuvujwa kwa rasilimali za umma kiholela.

    Baadhi ya viongozi mashuhuri wa CPC ambao wametembelea Kenya hivi karibuni ni pamoja na mwenyekiti wa jukwaa la ushauri la China CPPCC Wang Yang na Prof Hu Jianhua, ambaye ni naibu mtendaji mkuu wa Shule ya Chama cha CPC katika jimbo la Guangxi.

    Wakati wa ziara zao, viongozi hao wawili walizungumzia siri ya mafanikio ya chama chao hasa katika kudumisha utulivu wa kisiasa, pamoja na kuafikia mafanikio na ukuaji wa uchumi.

    Pia walisisitiza umuhimu wa kujitolea, nidhamu na utiifu kwa chama kama nguzo ya kuafikia malengo yoyote.

    Kabla ya kumalizika kwa ziara yake ya Kenya, mwenyekiti wa CPPCC Wang Yang alitangaza nia ya CPC ya kusaidia Jubilee katika kuanzisha shule ya chama. Pia aliahidi msaada kwa kujenga uwezo miongoni mwa viongozi wa chama hicho tawala.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako