Na Eric Biegon - NAIROBI
Makampuni ya Kichina yanayofanya kazi nchini Kenya yamefungua milango ya nafasi zaidi za ajira kwa wenyeji. Makampuni haya yalitangaza kuwepo kwa nafasi za ajira wakati Muungano wa uchumi na biashara kati ya China na Kenya ulipozindua rasmi maonyesho ya kazi kwenye jumba la KICC jijini Nairobi.
Hata ingawa lilikuwa tukio lililofanyika kwa mara ya kwanza, onyesho hilo lilivutia mamia ya wale wanaotafuta kazi ambao walikuwa ni pamoja na waliohitimu vyuo vikuu na vijana ambao wamekusanya uzoefu katika taaluma mbalimbali ambao walifika kwa wingi kwenye maonyesho hayo.
Zaidi ya makampuni 50 ya Kichina yalitoa maelezo yao ya ushirika kwa wenjeji wanaotafuta ajira. Baadaye ilibainika kuwa zaidi ya nafasi za kazi 1,000 zilikuwa wazi kwa Wakenya katika makampuni ya Kichina yanayoendesha shughuli zao nchini humo kwa sasa.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, mwakilishi wa Ubalozi wa China nchini Kenya Li Xuhang, alisema makampuni ya Kichina yanatazamia kuajiri Wakenya walio na taaluma pamoja na shauku ya kufanya kazi kwa bidii.
Alibainisha kuwa kwa kutegemea uwezo huu na ustadi mkubwa wa wafanyakazi wa ndani na wale wa Kichina, kampuni kama vile China Road and Bridge Corporation (CRBC) imeweza kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kama ilivyoratibiwa. Aidha anasema kampuni ya ujenzi ya Kichina ya AVIC International pia imefaulu kujenga ghorofa moja ya kituo cha biashara duniani kwa rekodi ya siku 10.
"Kwa niaba ya muungano wa KCETA iliyoandaa maonyesho ya kazi, tunawahamasisha wenyeji kutumia fursa hii na kuomba kupata nafasi za ajira zaidi ya 1000 zilizotolewa, zikiwa ni pamoja na nafasi tatu kwenye Ubalozi wa China," Bwana Li Xuhang alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa maswala ya Asia na Australasia kwenye Wizara ya Mambo ya nje ya Kenya Balozi Christopher Chika, amekaribisha hatua hiyo ya makampuni ya Kichina akisema hii inadhihirisha wazi dhamira ya kukuza mahusiano baina ya China na Kenya.
Kwa mujibu wa Chika, maonyesho ya kazi yatachukua nafasi nzuri katika kuvunja vikwazo vya kitamaduni huku yakijenga madaraja kati ya wanaotafuta ajira na makampuni ya kuajiri.
"Kenya imedumisha uhusiano wa kimkakati na China, kama inavyoonekana kupitia mwingiliano wa mara kwa mara kati ya viongozi kutoka mataifa hayo mawili. Katika safu ya kiuchumi, zaidi ya makampuni 400 ya Kichina yamekuwa yakitoa ajira pamoja na kuwezesha wenyeji kupata ujuzi wa kuwezesha ajenda ya maendeleo nchini Kenya,"alisema.
Akizungumza kwa niaba ya makampuni yote ya Kichina yaliyokuwepo kwenye maonyesho hayo, Wang Yantao kutoka kampuni ya SinoHydro alisema kuwa makampuni ya Kichina daima huweka umuhimu mkubwa kwa utoaji wa nafasi za ajira kwa wenyeji, hii ikiwa ni sehemu kubwa ya majukumu yake ya ushirika kwa jamii.
"Naamini wafanyakazi wa Kenya na wenzao kutoka China wana ndoto sawa ya siku za baadaye. Tutafanya kazi kwa pamoja ili kushinda changamoto za vikwazo vya lugha na utamaduni, kuyafuata sheria na kanuni zote husika, pamoja na kukuza ushirikiano mzuri wa kudumu baina ya nchi hizi mbili," alisema Wang.
Baadhi ya makampuni makubwa yaliyokushiriki ni pamoja na China Road and Bridge Corporation, Sinohydro Corporation, Huawei Technologies, na AVIC International miongoni mwa mengine.
Makampuni hayo yanashughulika katika sekta mbalimbali ya viwanda kama vile ujenzi, teknologia, magari, madini, vyombo vya Habari na sekta zinazohusiana kiuchumi.
KCETA ni shirika lisilo la kutafuta faida yenye wanachama 97 ambazo ni makampuni za Kichina. Muungano huo unalenga kuchunguza ushirikiano wa biashara kati ya China na Kenya na kuinua ubadilishanaji wa utamaduni, huku ukitekeleza majukumu ya kijamii na kukuza mshikamano wa jamii.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |