Na Eric Biegon - NAIROBI
Enzi mpya ya urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika inaendelea kushuhudiwa barani humo. Pande zote mbili yanapiga hatua muhimu katika mahusiano ya kibiashara pamoja na ubadilishanaji wa utamaduni na mahusiano ya watu kwa watu.
Katika nyakati za hivi karibuni, Afrika imekuwa kituo cha makampuni ya Kichina ambayo yanawekeza katika mataifa ya nje. Kote barani, makampuni ya Kichina yameleta ajira, mafunzo, teknolojia mpya na ufadhili wa miradi mbali mbali.
Kwa kufanya hivyo, hatua kwa hatua China inajaza mapengo makubwa katika maeneo kadhaa ya utekelezaji. Hatua hizi kwa upande mwingine zimesaidia kuinua viwango vya maisha katika Jamii mbalimbali hasa wakati makampuni hizi zinapotekeleza majukumu kwa jamii zilizoko maeneo wanamohudumu.
Manufaa hizi ni dhahiri nchini Kenya ambapo zaidi ya makampuni 400 ya Kichina yanahudumu kwa sasa. Bila shaka hali ya sasa inaonyesha kuwa makampuni haya yana nia ya kuwezesha jamii maskini katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Kampuni ya Kichina ya Twyford Ceramics, inayohusika na utengenezaji wa vigae vya ujenzi, kwa mfano, ilizindua oparesheni miaka miwili tu iliyopita katika kaunti ya Kajiado, eneo iliyoko kusini mwa mji mkuu wa Nairobi. Eneo hilo linamilikiwa na jamii ya wamaasai ambao ni wafugaji.
Ili kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa eneo hili, kampuni hiyo ilizindua mpango wa udhamini wa masomo wa "Maisha Bora" ambapo wanafunzi kutoka familia maskini watafaidika na ufadhili wa masomo kutoka kampuni hiyo.
Sawia na makampuni mengine ya Kichina yanayowekeza nchini Kenya, Twyford Ceramics Limited ilitoa ufadhili wa masomo ya kima ya shilingi nusu milioni kwa wanafunzi 35 kutoka eneo hilo mwaka uliopita.
Kupitia kampuni tanzu ya KEDA Ceramics Limited, kampuni hiyo ilizindua mpango huo wa udhamini, ili kulipa ada ya masomo kwa wasomi wasiojiweza kutoka vijiji vyote zilizopo eneo hilo.
Baadhi ya walionufaika na udhamini huo hawakuweza kuficha furaha zao. Mmoja baada ya mwingine wanafunzi hao walitoa shukrani zao kwa mkono wa msaada uliotolwa na kampuni hiyo.
"Tunawashukuru Twyford Ceramics Ltd kwa kutusaidia kutimiza ndoto zetu. Kampuni hiyo imefadhili sehemu kubwa ya ada ya masomo kwa miaka miwili mfululizo tangu nilipojiunga na chuo kikuu. Ninahisi vizuri sana." alisema mmoja wa wasichana walionufaika.
Matamshi yake yaliungwa mkono na mmoja wa viongozi wa mitaa ambaye alisema udhamini huo utatoa msukumo kwa vijana wengi kutoka jamii ya wafugaji wa kuendeleza elimu.
Kwa mujibu wa Johnstone Mpuki, ambaye ni mshirikishi wa kijamii katika kampuni hiyo, mpango huo wa masomo unalenga kubadilisha maisha ya vijana kutoka jamii ya Wamasai ambao bado wamekwama katika tamaduni zilizopitwa na wakati na umaskini.
"Lengo letu limekuwa kuwafikia watoto kutoka familia yasiyo na uwezo ambao ndoto yao elimu bora imedidimizwa kutokana na umaskini uliokithiri pamoja na desturi ya utamaduni uliojaa madhara kama ndoa za utotoni," alisema Akipongeza mpango huo kama hatua ya kuleta mwamko mpya, mshauri wa maswala ya uchumi na biashara katika ubalozi wa China nchini Kenya Guo Ce alisema jukumu hili hasa uhimizwa kwa makampuni ya Kichina yanayoendesha bishara zao nje ya nchi.
Alisema serikali yake itaendelea kupanua ushirikiano wake na Nairobi kwa kusaidia ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi katika ngazi za chini. Bwana Guo alisema makampuni ya Kichina hayana budi ila yaweke msingi katika nchi za nje wa kuchangia mipango ya maendeleo katika maeneo wanamohudumu.
"Serikali ya China inahimiza makampuni ya Kichina yanayohudumu nje ya nchi kuzingatia sheria na kujitwika shughuli za kijamii na kusaidia wananchi," alisema
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |