Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam
TANZANIA imeishukuru Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking cha China kwa kukubali ombi lake la kuanzisha ushirikiano na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Ushirikiano huo utaiwezesha Hospitali ya MOI ya jijini Dar es Salaam kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania ambao wamekuwa wakikosa huduma hiyo ama kulazimika kutumia gharama kubwa kwenda nje ya nchi.
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli akizungumza na Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking (PUIH), Prof Zhao Yuanil jijin Dar es Salaam, alisema ushirikiano huo utakuwa wa manufaa mkubwa kwa taifa ilo la Afrika ya Mashariki.
Prof. Zhao aliongozana na timu ya wataalamu wanaoshirikiana na Taasisi ya MOI.
Mazungumzo ya timu ya wataalam kutoka China na Rais Magufuli pia yalihudhuriwa na Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke.
Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli alimhakikishia Prof Zhao kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano zaidi utakaowezesha MOI kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania ambao wamekuwa wakikosa huduma hiyo ama kulazimika kutumia gharama kubwa kwenda nje ya nchi.
Rais Magufuli alielezea kufurahishwa kwake na taarifa za kufanyika kwa mafanikio kwa upasuaji wa kwanza uliofanywa na Dkt Bingwa Prof. Zhao hapo hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Dkt Magufuli alisisitiza kwamba anaamini wataalamu zaidi wataendelea kuja nchini Tanzania kutoka PUIH kwa ajili ya kutoa huduma na kuwafundisha madaktari wa Tanzania, na pia Watanzania wengi watakwenda nchini China kujifunza upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Kwa upande wake Prof. Zhao alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake kubwa za kuhakikisha Taasisi ya MOI inaimarishwa ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu.
Alieleza kuwa PUIH itahakikisha makubaliano yaliyotiwa saini mwaka jana kati ya hospitali hiyo na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yanatekelezwa kikamilifu.
"Tanzania kuna watu zaidi ya Milioni 50 na kuna idadi kubwa ya watu wenye magonjwa ya ubongo, wanaopata majeraha kichwani, uvimbe wa ubongo, matatizo ya mishipa ya damu ya ubongo na magonjwa ya uti wa mgongo ambao wanahitaji kupata matibabu mazuri hapahapa, lakini naambiwa kuna wataalamu 10 tu ambao hawatoshelezi mahitaji, ndio maana tupo hapa kuangalia mnafanya nini na tuone namna ya kusaidia kuwaongezea uwezo" amesema Prof Zhao.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface alisema kupitia ushirikiano huo Tanzania inatarajia kupata wataalamu wengi wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Picha: Rais John Magufuli akisalimiana na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Prof Zhao Yuanil kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu Cha Peking cha Beijing, China.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |