Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam
BUNGE la Umma la China linaanza vikao vyake mapema mwezi wa tatu. Ni mkutano muhimu unaojadili masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji wa shughuli za kiserikali, programu na malengo mbali ya nchi hiyo.
Bunge ilo linaketi miezi michache baada ya China kufanya maadhimisho ya miaka 40 tangu nchi hiyo ianze kutekeleza Sera ya Mageuzi na Ufunguaji Milango.
Hii ni sera ambayo iliweza kuipa China matokeo chanya hasa katika nyanja ya maendeleo, uimarishwaji wa diplomasia ya kiuchumi, mahusiano ya kimataifa pamoja na kuchochea shughuli za uwekezaji ndani na nje ya nchi.
Ni dhahiri kuwa, mkutano wa Bunge la Umma la China wa Mwaka huu, 2019, pamoja na mambo mengine itapokea taarifa mbalimbali juu ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayotoa miongozo ya namna bora ya kuiendesha serikali.
Sera ya Mageuzi na Ufunguaji Mlango, ulioasisiwa miaka 40 iliyopita imekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya China--- ambayo kwa sasa ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa, baada ya Marekani.
Mkutano wa Bunge wa mwaka uliopita, 2018, ambao kimsingi ulifanya mambo makuu mawili, pamoja na mambo mengine --kupitisha mabadiliko ya Katiba iliyoondoa ukomo katika nafasi ya urais pamoja kufanya uchaguzi wa viongozi wakuu wa taifa ilo la Asia Mashariki.
Katika mkutano uliopita, wawakilishi wa Bunge la Umma la China walipata pia kuelezwa hatua mbali mbali zilizofikiwa na serikali katika vita dhidi ya umaskini, ambapo mikakati iliwekwa bayana juu ya namna ambavyo serikali imejipanga kuondoa Wachina takribani milioni 30 katika lindi la umaskini.
Katika moja ya mipango iliyoelezwa mbele ya wajumbe wa Bunge hilo ni kuwa had kufikia mwaka 2020, nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu duniani, itakuwa imefanikiwa kuondoka na umaskini.
Bunge linapokaa mwezi wa tatu, mwaka mmoja kabla ya lengo la kuondokana na umaskini kufikiwa, ni dhahiri kuwa takwimu za wananchi waliondolewa katika janga hili litawekwa wazi.
Taarifa hizi pia zitakuwa chachu kwa nchi zingine ambazo zimedhamiria kupambana na umaskini, ikiwa ni moja kati ya malengo yaliyomo kwenye agenda ya Umoja wa Mataifa (UN) ya Maendeleo Endelevu 2030.
Licha ya Bunge la Umma la China kukaa mara moja tu kwa mwaka, tofauti na mataifa mengine ambayo hufanya mikutano kama hiyo hadi mara nne kwa mwaka, chombo hicho chenye maamuzi ya juu na ya mwisho kabisa inategemewa kujadili na kupitisha mambo mbalimbali.
Kama ilivyo ada, pamoja na mambo mengine yatakayojadiliwa ni, suala la mahusiano ya China na mataifa mengine duniani.
Mwaka jana, Baraza la Mashauriano la Kisiasa, ikitoa ripoti ya kazi kwa vipindi vilivyopita, liliweka bayana kuwa lilifanyia tathmini mfumo wa mahusiano yake na mataifa mengine na kuangalia namna ya kuboresha mahusiano hayo ili yawe bora zaidi.
Suala la diplomasia kwa sasa ni moja ya mambo mtambuka katika uendeshwaji wa mambo mbalimbali ya nchi, ikiwa kila nchi inataka kuweka vizuri sura yake na jinsi inavyotazamwa na mataifa mengine kwa namna ambayo itatoa mtazamo chanya.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |