Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM
BIDHAA zisizo na ubora imekuwa changamoto kubwa kwa nchi mbalimbali duniani hususan katika ukanda wa Afrika kwa kiasi fulani bidhaa hizo zimekuwa zikiingia au kutengenezwa kwa wingi.
Licha ya kuwepo kwa taasisi mbalimbali za udhibiti ubora wa bidhaa, bado changamoto kubwa imekuwepo hususan katika bidhaa za nguo, vifaa vya umeme, vifaa vya ujenzi na mengineyo, ikielezwa kupitiswa kwa mipaka isiyo rasmi.
Ikiwa ni miaka takribani 40 tangu China ifungue milango ya Nyanja mbalimbali za biashara huku ikiwa ya pili kwa utajiri na inayoongoza kwa idadi kubwa ya watu duniani, imekuwa ikiweka mkazo katika uwekezaji na kufanya biashara.
Shirika la Biashara Duniani, linaitaja China kuwa inaongoza kwa uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kuanzia mwaka 2009, jambo ambalo linadhihirisha umakini katika kufanya biashara.
Katika kukabiliana na Changamoto hiyo, Nje ya Mkutano wa Bunge la Umma uliofanyika mwanzoni mwa mwezi huu, nchi hiyo imejipambanua kuongeza adhabu kwa wazalishaji na wauzaji wa bidhaa zisizo na ubora nchini humo.
China imeonya kuwa itawaadhibu vikali wale wanaojihusisha na ukiukaji wa sheria za haki miliki na usambazaji wa bidhaa bandia. Mkuu wa utawala wa kanuni za soko nchini humo Zhang Mao alieleza kuwa serikali haitamwacha yeyote atakayevunja sheria.
"Tutahakikisha kuwa wazalishaji na wauzaji wa bidhaa bandia wanaadhibiwa kwa vitendo vyao vya uhalifu ipasavyo, hata kufilisiwa ." Zhang aliwaambia waandishi wa habari pembeni mwa vikao vinavyoendelea vya mikutano mikuu ya bunge nchini humo.
Kwa mujibu wa Zhang, utawala wake utafichua kwa umma wote wanaoendeleza maovu haya huku akionya kuwa "wao hawana nafasi ya kujificha chini ya jua."
Alisema pia wanapanga kupunguza idadi ya bidhaa bandia na kumaliza hali ya wasiwasi miongoni mwa raia kuhusu bidhaa hizo.
Wakati huo huo, Zhang alibainisha kuwa China inashinikiza kuwepo kwa udhibiti wa kampuni za ndani kwa nia ya kukuza na kuimarisha mfumo wa mikopo ya kijamii.
Wiki hii, Katika kuhakikisha malengo yanafikiwa ya kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisiszo na ubora Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Viwango la China (CCIC) wamekubaliana kushirikiana.
Katika makubaliano hayo yaliyofanyika ubalozi wa Tanzania, Beijing China watendaji wa taasisi hizo walikutana na kufanya mazungumzo na hatimaye kusaini makubaliano hayo.
Ni dhahiri kuwa kwa makubaliano hayo ya pande mbili, yatasaidia kuwadhibiti wafanyabiashara wenye uchu wa kupata faida na kusafirisha bidhaa zisizo na ubora kwa kuhakikisha watendaji mipakani na njia mbalimbali za usafiri wanapambana bila kuchoka kufikia malengo ya nchi hizi rafiki kwa takribani miaka 50 sasa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |