Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya reli Tanzania na Zambia (Tazara) inayosimamia reli hiyo ya kihistoria baina ya nchi za Afrika na China kutokana na China kukubali kujenga reli hiyo kati ya mwaka 1970 mpaka 1975.
Reli hiyo licha ya kusaidia kupatikana kwa uhuru kwa nchi za kusini mwa Afrika kwa kusaidiwa na nchi za Afrika Mashariki hususan Tanzania katika Nyanja mbalimbali imesaidia kukuza uchumi wa nchi hizo kwa kusafirisha mizigo na abiria baina ya pande hizo mbili.
Reli hiyo yenye mafanikio lukuki katika siku za karibuni imeshuhudia kuporomoka katika uwezo wa kuendesha shughuli zake kwani mwaka 1976 wakati wa uanzishwaji wake lilikuwa na uwezo wa kubeba mizigo ya tani milioni 5 kwa mwaka wlakini kwa sasa ina uwezo wa kubeba tani si zaidi ya 128,000 tu kwa mwaka 2016.
Hivi karibuni Mkurugenzi mkuu wa Tazara Bruno Ching'andu anasema wameanza kupaa matumaini ya kurudi katika hali yake ya kawaida baada ya kuanza kufanya vizuri katika baadhi ya sehemu.
Anaeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu (2015/2016 hadi June 2018), yameongezeka kwa mizigo iliyosafirishwa kimeongezeka kutoka tani 88,000 hadi tani 220,000. huku wakilenga katika kipindi cha miezi 18 hadi 24 ijayo kufikia lengo la kusafirisha tani 600,000 kwa mwaka kama mipango itaenda kama walivyoweka.
Abiria waliotumia treni hiyo mwaka 2017 walikuwa milioni 2.37 na wameongezeka hadi kufikia 2.42 milioni Juni 2018.
Lakini kumekuwa na mikakati zaidi ya uboreshaji wa reli hiyo baada ya kukamilika kwa ripoti ya pili ya upembuzi yakinifu huku China ikiwa tayari kutoa fedha za kuboresha reli hiyo.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Tazara, Timothy Kayani anasema katika uboreshaji, Tanzania na Zambia waliiomba China kusaidia kupata kampuni ya kufanya utafiti ili kubaini matatizo na mwongozo utakaotumika kuboresha.
Anasema, China iliiteua kampuni ya Railway Survey and Design Institute (TSDI) iliyofanya upembuzi huo kwa mwaka mmoja na kuwasilisha ripoti ambayo baada ya Zambia na Tanzania kujadili ilikuwa na mapungufu na kuomba China kupitia upya.
Amebainisha kuwa, kampuni hiyo iliendelea na mchakato na sasa wameishakabidhi ripoti ya pili ambayo itajadiliwa na pande zote ikifikiwa mwafaka itafanyiwa kazi na uboreshaji kuanza.
"China imekubali kuboresha reli hii, lakini bado kuna makubaliano yanatakiwa kufikiwa na Tanzania, Zambia na China kwa kutumia ripoti hii ili uboreshaji kuanza." anasema.
Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke akizungumza wakati wa kumbukumbu ya raia wa China waliokufa wakati wa ujenzi wa Tazara wiki iliyopita alibainisha kuwa kuwa nchi yake iko tayari kuboresha reli hiyo ambayo ni alama ya ushirikiano kati ya China na Afrika.
Anasema wanasubiri kukamilika kwa majadiliano na michakato baina ya Zambia na Tanzania kuhusu uboreshaji huo ili kuanza kazi.
Pia, Kayani anasema katika fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania Sh bilioni 10 kuboresha reli hiyo zimenunua vipuri vinavyotarajiwa kuwasili mwezi huu.
Alieleza kuwa, fedha kama hizo zinatakiwa kutolewa pia na Zambia kwa kuwa ni makubaliano katika kuboresha reli hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi hizo mbili.
Mei mwaka jana, Tanzania ilitoa Sh bilioni kumi kwa ajili ya kuboresha reli ya Tazara nchini ili iweze kujiendesha kwa kusafirisha mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia, kuzalisha faida na kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa kwa nchi mbili.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alisema fedha hizo zitatumika kununua traction motors saba zenye gharama Sh bilioni 7 kwa ajili ya kufunga kwenye injini 42 za vichwa vya treni ili kuhakikisha kuwa treni inasafiri kwa usalama na kwa uhakika kutoka eneo moja kwenda lingine bila kuharibika njiani na kuchelewesha safari za abiria au mizigo ya wateja ambapo itaboresha utendaji kazi wa Tazara na hivyo kuongeza makusanyo ya mapato yake.
Anafafanua kuwa, fedha nyingine kiasi cha Sh bilioni 3 zitatumika kununua mtambo na vitendea kazi kwa ajili ya kiwanda cha kutengeneza kokoto cha Tazara ambapo kokoto hizo zinatumika kuimarisha njia ya reli ya Tazara na miundombinu yake, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kuota kwa nyasi na kupunguza mtetemo wakati wa safari.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |