Majaliwa Christopher, Dar es Salaam
SERIKALI ya China imekubali kutoa msaada wa Dola za Kimarekani million 24.2 (Shilingi Bilioni 56 za Tanzania) kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Cha Taifa cha Ulinzi Tanzania awamu ya pili.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Dkt. Hussein Mwinyi alisema jana Jumanne, Aprili 16, 2019, kuwa msaada huo kupitia Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China utasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wa kozi fupi na ndefu kwa mafunzo ya viwango vya kimataifa.
Waziri Mwinyi alisema hayo wakati wa uwekaji jiwe la msingi la kuanza ujenzi huo utakaotekelezwa ndani ya miezi 15 katika eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Waziri Mwinyi alitoa shukrani kwa ushirikiano na msaada unaoendelea kutolewa na nchi hiyo ya Asia ya Mashariki.
Chuo hicho kinajengwa na kampuni ya First Group Construction ya nchini China, ili kiweze kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi wa kijeshi.
"Kwa niaba ya serikali ya Tanzania, naishukuru serikali ya China kwa kutupatia msaada wa kutujengea Chuo cha Kijeshi chenye hadhi na viwango vya kimataifa, kwani lengo letu ni kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi kulinganisha na hapo awali," alisema Dkt. Mwinyi.
Vilevile, Waziri huyo alipongeza China ambayo ni nchi ya pili kwa utajiri duniani, kwa kuchukua jukumu la kujenga Wizara ya Ulinzi kwenye mji wa serikali uliopo jijini Dodoma.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alisema chuo hicho kitakachotoa mafunzo ya ulinzi wa taifa kwa maofisa wa jeshi na Serikali, ni sehemu ya misaada ya China kuliimarisha jeshi la Tanzania liwe la kimataifa.
Alisema baada ya kukamilika kwa mradi huo, zaidi ya wanafunzi 100 wataweza kusajiliwa katika nyanja mbalimbali tofauti na ilivyokuwa awali ambapo wanafunzi 40 tu ndo waliweza kupokelewa katika muhula mmoja.
"Lakini hivi karibuni China wametukabidhi Jengo la chuo cha mafunzo maalumu Bagamoyo na wametuahidi kutujengea makao makuu ya jeshi kule Dodoma na ujenzi utaanza hapo baadaye," alisema Jenerali Mabeyo.
Aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuwapa msaada wa kifedha kwa ajili ya kuendeleza mafunzo ya kijeshi, ili kuhakikisha nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki inakuwa kwenye viwango vya kimataifa.
"Tanzania tunahitaji idadi kubwa ya wanajeshi wenye ujuzi, hivyo ninaamini kwa msaada wanaotupatia China, vijana wengi watapata mafunzo yenye viwango vya kimataifa," alisema Mabeyo.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke alisema mahusiano ya Tanzania na China yanaendelea kuimarika zaidi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini.
Aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |