Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam
KUFATIA mkataba wa kuuziana zao la mihogo kusainiwa kati ya Tanzania na China mwaka 2017 jijini Beijing, jumla ya viwanda vitano vya kuchakata zao hilo vimejengwa katika nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Bw. Joseph Kakunda amesema mpaka sasa kuna viwanda vitano ambavyo vimejengwa katika mikoa ya Pwani na Tanga na vimejengwa na raia wa China.
Alisema mkoani Pwani kuna viwanda viwili na Tanga viwanda vitatu.
Bw. Kakunda alisema viwanda hivyo vitakuwa vikichakata mihogo wanayoinunua kutoka kwa wakulima na kisha kuisafirisha kwenda nchini China.
Hadi sasa, kwa mujibu wa taarifa kutoka wizara hiyo iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wake wa zamani, Charles Mwijage, Tanzania ilipata soko la mihogo la tani milioni mbili katika nchi hiyo ya Asia ya Mashariki.
Mwijage alisema soko hilo kama litatumiwa vizuri, litaiingizia Taifa Dola za Marekani milioni 300 sawa na Shilingi bilioni 691, huku tani moja ya mihogo ikiuzwa kwa Dola za Marekani 150 ambayo ni zaidi ya Shilingi 300, 000 za Kitanzania
Alisema uzalishaji wa zao hilo nchini Tanzania bado uko chini kwa kuwa hekta moja inatoa tani tatu ikilinganishwa na China ambako hekta moja inatoa tani 50.
Alisema kwa Afrika, Nigeria inaongoza kwa kuuza tani milioni 44 za mihogo nchini China kwa mwaka.
Katika hilo, Waziri Kakunda alisema ndani ya miaka miwili kuanzia sasa, Tanzania itakuwa na uwezo wa kuuza tani milioni moja za mihogo nchini China.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. Edwin Lutageruka alisema tofauti na miaka iliyopita, hivi sasa mwamko wa Watanzania katika kuchangamkia soko hilo la mihogo nchini China umekuwa mkubwa.
Lutageruka alisema kuna kampuni sita za China hapa nchini katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga zinazonunua mihogo kutoka kwa wakulima na kuichakata kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
Alisema Januari mwaka huu, 2019, walikuwa na kikao na wadau wa zao la mhogo na miongoni mwa mambo waliyojadiliana ni kuanzisha chama cha wadau hao ambacho alisema kipo kwenye mchakato wa kupata usajili kama mkakati wa kuhakikisha wananchi na Taifa wananufaika na soko hilo la mihogo.
Kwa mujibu wa Lutageruka, zao la mhogo linalimwa takribani nchi nzima, lakini hasa katika mikoa ya Pwani ukiwemo Pwani, Mtwara, Lindi, Tanga na Morogoro.
Novemba 2017, akihutubia kwenye sherehe za 68 za Siku ya Taifa la China kwenye Ubalozi wa China nchini, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Susan Kolimba alisema Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zilisaini makubaliano yaliyofungua masoko ya China kwa ajili ya mihogo mikavu kutoka Tanzania.
Dkt. Kolimba alisema kupitia makubaliano hayo, kulikuwa na mazungumzo kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Kichina ya Wuxi Goodways International Trade Co, Ltd (WGIT) kwa ajili ya kusafirisha mihogo kutoka Tanzania kwenda China.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |