Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam
WATAALAMU wa Jiolojia kutoka nchini China wanashirikiana na wenzao wa Tanzania kujadili namna bora ya kuboresha sekta ya madini katika nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.
Wataalamu hao kutoka Asia ya Mashariki walitoa jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili, Aprili 28, 2019, kwa mazungumzo ya siku tano.
Wakiongozwa na Naibu wa Waziri wa Maliasili, Bw. Mr Zhong Ziran, wataalamu hao wa China watabadilishana utaalamu juu ya mambo mbalimbali yanayohusu usimamizi wa madini.
Naibu waziri wa Madini wa Tanzania, Bw. Stanslaus Nyongo amesema ujio wa wataalamu hao kutoka China umetokea wakati nchi hiyo iko katika mageuzi makubwa ya sekta ya madini ambayo ni moja ya sekta zinazoongoza kuingizia Tanzania fedha za kigeni.
"Huu ushirikiano kati ya China na Tanzania katika sekta ya madini utasaidia Tanzania kuwa na uwezo wa kufanya tafiti mbalimbali za kijiolojia ili kutambua kiasi na aina ya madini yaliyopo nchini na namna ya kuyaongezea thamani kwa ajili ya kupata soko imara na la uhakika," alisema Bw, Nyongo.
Alisema hivi karibuni serikali ya Tanzania ilifanya maboresho na mapitio ya sheria na sera mbalimbali za madini ili kuendana na mazingira ya sasa na kuwezesha nchi kufaidika zaidi na maliasili hiyo.
Madini yanayopatikana nchini Tanzania ni pamoja na dhahabu, almasi, Tanzanite, silva, chuma, kobati na graphite.
Aliongeza kuwa kutoka na dira ya serikali kulenga uchumi wa kati na wa viwanda, wizara ya madini kwa sasa imejikita katika mikakati mbalimbali ya ushirikiano kwenye miradi mikubwa ya maliasili ya madini nchini.
Naibu waziri wa Maliasili wa China Bw. Zhong alisema kuwa China na Tanzania watashirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Tanzania, kufanya utafiti pamoja na kubadilishana uwezo kwenye teknolojia.
"Tutaendelea kushirikiana katika kutoa mafunzo kwa wataalamu wa madini wa Tanzania, kufanya utafiti na pia kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa," alisema Bw. Zhong.
Tanzania ni tajiri kwa kubahatika kuwa na madini ya kila namna na hivyo uchimbaji na uwekezaji wake umekuwa ukiongezeka kila mwaka.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |