Na Eric Biegon – NAIROBI
Wakulima wadogo wadogo kutoka Kenya wamo mbioni kufaidi kutokana na uamuzi wa China kufungua soko lake kwa bidhaa za kilimo kutoka taifa hilo la Afrika Mashariki. Miongoni mwa mimea mengine, Beijing iliingia makubaliano na Nairobi mwezi Novemba mwaka jana ambapo mazao ya maembe, korosho na parachichi zitaingia katika soko la China kwa mara ya kwanza.
Tangu maafikiano hayo, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ilianzishwa mchakato wa kusaidia kupiga jeki sekta ya kilimo ya parachichi na kuhakikisha kuwa imetimiza matakwa ya kimataifa kikamilifu.
Tayari, sheria za usafirishaji nje wa parachichi umewekwa wazi na mamlaka ya China. Haina ya parachichi ijulikanayo kama Hass ndilo lililoruhusiwa kuingia soko la China.
Na kwa sababu ni wakulima wachache tu ambao wana uwezo wa kupata aina hii ya parachichi, serikali ya Kenya imeingilia kati ili kuwasaidia wakulima kupata zao hilo kwa ajili ya kupanda kabla ya kusajiliwa katika kundi ambalo litakuwa likisafirisha nje tunda hilo.
Wakulima zaidi ya 1500 kutoka kata 35 katika Kaunti ya Murang'a walinufaika na miche inayohitajika wiki hii wakati serikali ya kaunti ilizindua mpango wa kusambaza miche ya haina hiyo ya parachichi ya Hass.
Gavana wa kaunti hiyo Mwangi Wa Iria alianzisha mkakati wa kuhamasisha wenyeji kuukumbatia kilimo ya parachichi kama njia ya kutokomeza umaskini pamoja na kukuza afya zao.
"Tumeanzisha rasmi usambazaji wa miche ya avokado. Tumeandaa miche 500,000 na tumeorodhesha wakulima 100,000 watakaofaidi kutokana naprogramu hii." Mkuu wa kilimo wa Murang'a Albert Mwaniki alisema
Hakika, Murang'a ni kaunti inayoongoza katika uzalishaji wa parachichi kote nchini Kenya. Kaunti hiyo inazalisha asilimia 70 ya avokado kwa ajili ya usafirishaji na matumizi ya ndani. Sasa kaunti hiyo ni nyumbani mwa parachichi aina Hass.
"Tunda hili likikomaa linabadili rangi ya ngozi kutoka kijani na kuwa zambarau ishara kwamba limeiva. Aina hii ya parachichi inaweza kuishi hadi mwezi mmoja nje ya friji. Haiwezi kuharibika kwa haraka. Na inafanya vizuri katika hali yoyote ya joto iliyowekwa." Mwaniki alifafanua.
Mamia ya wakulima ambao walijaza ukumbi wa usambazaji wa miche hiyo ni wale ambao walihama kutoka ukulima wa kahawa hadi kilimo cha parachichi.
Tofauti na kahawa na chai, mkulima mmoja alibainisha kwamba aliamua kujiunga na mradi huu mpya kwa sababu "miti ya avokado inahitaji huduma cha kiwango cha chini na ilihali matunda yake yana faida nyingi."
Ama kwa kweli, wakulima hao wanafichua kuwa walibadilisha kilimo chao cha kahawa na chai kwa ajili ya parachichi katika jitihada za faida hasa zinazotokana na kuongezeka kwa hitaji lake nchini China.
"Mimi nimekuwa nikitafakari mno kuhusu kujihusisha na kilimo cha parachichi kwa sababu za kiuchumi. Awali sikujua aina ambayo ningepanda lakini sasa nimepewa miche 20 ya Hass ya kuanzisha kilimo hii. Nimeambiwa hii ndiyo iliyoruhusiwa katika soko la China na kwa hakika ninasubiri kufaidika kifedha kutokana na upanzi wake." Mkulima Gichane Njae alibainisha.
Kwa mujibu wa uongozi wa kaunti ambao ndio uliitisha mkutano katika uwanja wa michezo wa Ihura, programu hii itainua kilimo na uchumi kwa kuwawezesha wakazi.
Uongozi wa kaunti hiyo umefichua kwamba programu hii itaendelezwa kwa awamu ambapo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu miche zaidi ya milioni 1 zitakuwa zimesambazwa kwa wakulima.
Kila mkulima alipata miche minne wakati wa uzinduzi wa shughuli hiyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |