Majaliwa Christopher, Dar es Salaam
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imetangaza jana mikakati mipya ya kuhakikisha inaendelea kupata watalii zaidi toka nchini China huku ikibainisha pia kuwa imejipanga kutangaza mazao ya misitu nchini humo ikiwemo asali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya TTB Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alisema kwamba viongozi kutoka nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki wamepanga kufanya ziara nchini China kwa ajili ya kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii katika nchi hiyo ya Asia ya Mashariki.
Jaji Mihayo alisema kuwa kiongozi wa msafara huo utakao ambatana maafisa mbalimbali kutoka TTB na wizara ya Utalii na Maliasili atakuwa ni Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki.
Alieleza kuwa ziara hiyo ya wiki moja nchini China itaanza mwezi Juni tarehe 19 hadi tarehe 26 katika miji minne.
Miji itakayotembelewa na ujumbe huo kutoka Tanzania kwa mujibu wa Jaji Mihayo ni Beijing, Shanghai, Nanjing na Shangsha, lengo pia likiwa ni kuhakikisha Tanzania inaongeza sehemu ya umiliki wa soko la utalii China.
Alisema katika ziara hiyo TTB inaambatana na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi na ya umma ikiwemo Tanapa, wakala wa huduma za misitu, Makumbusho ya taifa, idara ya mambo ya kale na mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori.
Jaji Mihayo aliongeza kuwa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) na vyanzo vingine vya habari habari duniani vimebainisha kuwa soko la utalii la China linaendelea kuongoza kuwa na idadi kubwa zaidi ya watalii na mchango mkubwa katika uchumi wa dunia.
"Kwa sababu hii TTB na wadau tuliona fursa kubwa ya kuongeza jitihada za kuwavutia watalii zaidi katika nchi hiyo ya Asia ya Mashariki," alisema Jaji Mihayo.
Hivi karibuni watalii 330 kutoka China waliwasili nchini Tanzania ambao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 ambao wanatarajiwa kutembelea Tanzania mwaka huu 2019, chini ya mpango unaosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |