• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Chuo Kikuu cha Taaluma za Lugha za Kimataifa Shanghai chaanza kufundisha shahada ya kwanza ya Kiswahili

    (GMT+08:00) 2019-06-14 08:47:42

    Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    KISWAHILI --moja ya lugha inayozungumzwa na watu wengi Afrika na nje ya bara hilo, imeendelea kuenea zaidi na kupata umaarufu, na sasa Chuo Kikuu cha cha Taaluma za Lugha za Kimataifa cha Shanghai (SISU) cha China, kimeanza kufundisha shahada ya kwanza ya Kiswahili.

    Chuo hicho ndicho cha kwanza katika ukanda huo wa Mashariki mwa China kufundisha shahada ya Kiswahili. Vilevile hatua hiyo imefanya Kiswahili kuwa lugha pekee kutoka barani Afrika kufundishwa chuoni hapo.

    Chuo Kikuu cha Taaluma za Lugha za Kimataifa cha Shanghai kinaungana na vyuo vingine nchini humo ambavyo tayari vilishaanza kufundisha lugha hiyo. Hivyo vyuo ni pamoja na Chuo cha Mawasiliano ya Habari cha China, Chuo kikuu cha Lugha za kigeni cha Beijing, na Chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Tianjin.

    Akizungumza katika kampasi kuu ya chuo hicho jijini Shanghai hivi karibuni, Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule Kuu ya Lugha za Asia na Afrika, Ma Jun alisema Kiswahili kina umuhimu wa pekee ndiyo maana imeanzishwa kozi maalumu ya Kiswahili katika mwaka huu wa masomo.

    Ma alijifunza lugha ya Kiswahili katika Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.

    Alisema kozi hiyo ina wanafunzi kumi ambao wapo katika mwaka wa kwanza na kwamba wanatarajia kupokea wanafunzi wengi zaidi.

    "Wanafunzi tulionao wote ni raia wa China. Lengo ni kuwafanya wazijue lugha za kimataifa kwa ufasaha na kuweza kurahisisha mawasiliano na mtangamano. Tumeona Kiswahili kinakua kwa kasi, nasi tumeona tusipitwe. Mbali ya Kiswahili wanafunzi hawa wanasoma pia juu ya uchumi, diplomasia, siasa, habari, utamaduni, Kiingereza na kadhalika.

    "Hawa wakihitimu baada ya miaka minne, tuna uhakika wataendelea kukuza Kiswahili katika sehemu nyingine hasa vyuoni. Usishangae kuona miaka michache ijayo Kiswahili kinapata umaarufu mkubwa hapa China," alisema Ma.

    Hata hivyo, alisema changamoto kubwa waliyonayo ni upatikanaji wa vitabu vya Kiswahili, hasa vinavyouzwa kwa njia ya mtandao.

    "Tuna mahitaji ya vitabu, lakini ni lazima uagize kitabu halisi na hapa kwetu kuna taratibu nyingi za kufuata, si rahisi. Ingependeza vingekuwa vinauzwa kwa njia ya mtandao," alisema. Kuhusu walimu, alisema wapo watatu, lakini wataajiri kadiri mahitaji yatakavyoongezeka.

    Kozi za Kiswahili katika vyuo vikuu China ilianza kufundishwa katika miaka ya 1960 na Chuo Kikuu cha Mawasiliano ya Habari China cha jijini Beijing. Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni Beijing nacho kilianza kufundisha mwaka 1961. Kingine ni Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tianjin.

    Kwa ujumla, Kiswahili, lugha ya Taifa ya Tanzania na ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 100 kote duniani, wengi wakiwa wa Afrika Mashariki, kinakua kwa kasi, na hadi sasa kimepitishwa kuwa moja ya lugha rasmi katika Umoja wa Afrika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako