Na Eric Biegon – NAIROBI
Kiongozi wa upinzani wa Kenya Raila Odinga alikuwa mwenyeji wa balozi wa China nchini Kenya Wu Peng katika ofisi yake ya Capitol Hill jijini Nairobi. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kitengo cha habari cha Odinga, wawili hao walibadilishana mawazo juu ya kuimarisha mahusiano yaliyomo kati ya Nairobi na Beijing.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyumba vya habari siku ya Jumatano, wawili hao pia walijadili njia za kujenga mahusiano imara kati ya Afrika na China.
"Walizungumzia mambo ya biashara, utamaduni na maendeleo ya miundombinu kama maeneo yaliyo na uwezo wa kuendeleza ushirikiano zaidi." Taarifa ilisema
Aidha, taarifa hiyo ilifichua kuwa Odinga, ambaye sasa ni mwakilishi mkuu wa maendeleo ya miundombinu wa Umoja wa Afrika (AU), alitoa wito kwa China kushirikiana na Kenya katika kuendeleza vituo vya kisasa vya michezo kama njia ya kuimarisha ushirikiano wa kiutamaduni.
Msemaji wa Odinga Dennis Onyango pia alibainisha kwamba Waziri Mkuu huyo wa zamani aliomba msaada wa China katika maendeleo ya sekta ya usafiri wa baharini ya Kenya ili kuinua biashara ya kanda na kuwekeza katika maendeleo ya kanda za kiuchumi maalum iliyopangwa kwa ajili ya sehemu mbalimbali za nchi.
Kwa upande wake, Balozi Wu Peng alimhakikishia Odinga kuwa China bado inanuia kukamilisha upanuzi wa njia ya reli ya kisasa ya SGR kutoka Naivasha kuelekea Kisumu na Malaba.
Ama kwa kweli, hakikisho hilo kutoka Balozi Wu lilitolewa huku kukiwa na ufunuo kutoka kwa Waziri wa uchukuzi James Macharia kwamba China inaelekea kukamilisha mipango ya ufadhili wa awamu ya pili (2B) ya ujenzi wa SGR hadi kwenye mpaka wa Kenya na Uganda.
"Ni kweli kwamba fedha zimeidhinishwa na Wizara ya biashara ya China na sasa zimo mikononi mwa Benki ya Exim ambayo ndiyo inayoangalia mienendo ya fedha ya mikopo kwa mujibu wa hali katika kila nchi." Macharia aliiambia chumba moja cha Habari nchini Kenya.
Taarifa hii inathibitisha zaidi kwamba suala la ufadhili wa awamu ya 2B ya SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu haikujadiliwa wakati wa mkutano uliokamilika mwezi Aprili wa Mkanda Moja Njia Moja jijini Beijing kama ilivyokuwa imetajwa kwenye vyombo vya habari. Kwa mujibu wa wakosoaji, China ilikataa kutoa mkopo kwa Kenya kukamilisha mradi huo.
Balozi Wu alibainisha kwamba mradi wa SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi kwa sasa unaendelea kufanikiwa na kupata mapato jinsi ilivyoratibiwa.
Hata ingawa yeye ni kinara wa upinzani nchini Kenya, Odinga kwa sasa anashirikiana kwa karibu na Rais Uhuru Kenyatta baada ya wawili hao kusitisha ugomvi baina yao na kutangaza makubaliano ya kufanya kazi kwa pamoja punde tu baada ya uchaguzi wa Rais wa mwaka 2017.
Azimio lao la kusitisha tofauti zao za kisiasa lilifungua njia ya Odinga kuteuliwa kama mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika. Baada ya uteuzi huo, Odinga aliahidi kutumia nafasi hiyo kusaidia bara la Afrika kuafikia malengo yake ya maendeleo.
Odinga, ambaye ni mhandisi, alisema anakusudia kufanya kazi kwa karibu na viongozi kutoka bara hilo anapoanza kazi ya kutafuta msaada kwa ajili ya miradi mikuu ya miundombinu ambayo baadhi yao yamekuwa yakipangwa kwa miaka mingi.
"Kwa msaada wa taasisi husika na ofisi ya tume ya Umoja wa Afrika na washirika wa bara hili, nitatumia nafasi yangu kushinikiza Afrika kutambua ndoto za waanzilishi wa nchi zetu ambao walitaka bara moja iliyounganika na inayojivunia usafirishaji wa bidhaa na wananchi wake kwa njia rahisi."alisema.
Baada ya kuhudumu awali kama Waziri wa barabara na ujenzi wa Kenya, Odinga alisema imani iliyoko katika uwezo wa miundombinu kusukuma ukuaji ndio sababu kuu yake yeye kukubali kuteuliwa na tume ya Umoja wa Afrika kwenye sekta hii.
"Ninaamini sasa kwamba kuwepo kwa miundombinu ya uhakika ya barabara na reli, kutoka kaskazini hadi kusini, Mashariki na magharibi ya Afrika, ni muhimu kwa kufungua bara na kuifanya njia ya kuingia karne ya 21." Odinga alisema.
Hadi sasa Odinga amesafari mara mbili kuelekea China tangu kuteuliwa kwake na ziara zake zinaonekana kuwa na umuhimu kwa Kenya na Afrika kuafikia maazimio yao ya miundombinu na matamanio ya maendeleo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |