• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Super Agri Technology ya China kuwekeza Dola Bilioni 1 sekta ya Kilimo Tanzania

    (GMT+08:00) 2019-07-01 09:50:28

    Na Majaliwa Christopher

    TANZANIA imeingia katika makubaliano mengine na kampuni kutoka Serikali ya Watu wa Jamhuri ya China kuwekeza katika sekta ya kilimo.

    Hatua hiyo inakuja huku takwimu za hivi karibuni zikionyesha kuwa nchi hiyo ya Asia Mashariki ambayo ni ya pili kwa utajiri duniani inabakia kuwa mbia mkubwa wa Tanzania katika uwekezaji na biashara.

    Hadi kufikia mwaka jana, biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia Dola za Kimarekani Bilioni 3.974.

    Mjini Changsha ambapo maonesho ya kwanza ya uchumi na biashara ya China na Afrika yamefanyika, Kampuni ya Super Agri Technology ya China imeingia makubaliano ya kuwekeza Dola 1 bilioni ndani ya miaka mitano nchini Tanzania.

    Uwekezaji huo utasaidia kuinua kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya sekta hiyo katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ikiwa ni mwendelezo wa kuvutia wawekezaji na kuongeza tija ya kilimo.

    Makubaliano hayo yameingiwa mwezi mmoja baada ya serikali ya Tanzania kushauri wawekezaji kutoka nchini China kuanza kuwekeza katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo kwa kuwa nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki ina utajiri mkubwa wa malighafi kwa ajili ya viwanda hivyo.

    Akizungumza na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchini China hivi karibuni jijni Arusha, Tanzania, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Bi. Angela Kairuki alisema idadi ya watu nchini Tanzania watakaokuwa wanaishi mijini itapanda hadi asilimia 50 kufikia mwaka 2050, hali inayosababisha kuwepo na uhitaji mkubwa kwenye uwekezaji katika sekta hiyo.

    Waziri Kairuki aliwaambia wafanyabiashara hao kuwa kutokana na makadirio hayo ya kuongezeka kwa idadi ya watu mijini, mahitaji ya chakula pia yatapanda kiasi kwamba uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo yatakuwa na tija kubwa.

    Maonesho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu ya "ushirikiano kuleta mafanikio ya pamoja, kuhimiza uhusiano wa uchumi na biashara kati ya China na Afrika", yalihusisha shughuli mbalimbali za biashara, uwekezaji, teknolojia za kilimo, nishati, maeneo ya ushirikiano ya viwanda, miundombinu na ushirikiano wa mitaji.

    Hatua hiyo ya kuingia makubaliano hayo imekuja baada ya mkurugenzi mkuu wa Mamlaka Ukanda wa Uwekezaji Tanzania (EPZA) Joseph Simbakalia kubainisha fursa zilizopo katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

    Kufanikisha uwekezaji huo: "Super Agri watashirikiana na (Ukanda wa Uwekezaji wa Kilimo Tanzania) Tanzania Agricultural Export Processig Zone (TAEPZ)" ilisema taarifa kutoka kwa taasisi hiyo.

    Makubaliano hayo yalifanyika Juni 28, 2019 kati ya kampuni hiyo na mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Lilian Ndosi na kushududiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi aliyehudhuria mkutano baina ya taasisi za fedha za China na mawaziri 53 wa mambo ya nje kutoka Afrika.

    Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Super Agri Technology itawekeza fedha hizo kwa kipindi cha miaka mitano.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako