Na Eric Biegon – NAIROBI
China imetoa ahadi ya kusaidia juhudi za Kenya za kutoa na kuchukua huduma za afya karibu na raia katika sehemu zote za nchi. Balozi wa China nchini Kenya Wu Peng alizungumzia kujitolea kwa Beijing kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha kwamba pande zote zinanufaika wakati mahusiano baina ya nchi hizo mbili zinaendelea kunawiri.
Akizungumza wakati alipomtembelea mama wa taifa wa Kenya Margaret Kenyatta katika ikulu ya Rais, Balozi Wu alifichua kwamba utawala wa Rais Xi Jinping kwa sasa "inachunguza maeneo ya ushirikiano ambayo yatawawezesha madaktari na wauguzi kutoka Kenya kupata mafunzo nchini China."
Hii kwa mujibu wa Balozi Wu, ni eneo la kupewa kipaumbele kwa sababu kuna haja ya kukuza na kuendeleza mafunzo ya wataalamu wa matabibu nchini Kenya na Afrika kwa ujumla.
Balozi Wu alimpongeza mama wa taifa kwa jitihada zake za muda mrefu katika kukuza mahusiano ya China na Kenya. Alisifu hatua zilizopigwa katika juhudi za Bi Kenyatta za kutaka kuboresha hali ya afya ya watu wa Kenya, hasa wanawake na watoto na kuhakikisha kwamba yamelindwa kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuiwa.
Mjumbe huyo kutoka China alimhakikishia Bi Margaret Kenyatta kuwa ubalozi wake utatoa usaidizi kwa ajili ya mpango huo wa "Beyond Zero."
Aliahidi kudumisha mawasiliano ya karibu na ushirikiano na mama wa taifa wakati wa utawala wake, na kukuza urafiki baina ya wa watu wa China na Afrika kikamilifu ili hatua kwa hatua Wakenya watimize malengo ya afya kwa wote ambayo ni moja ya ajenda nne kubwa za serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.
Bi Margaret Kenyatta aliishukuru China kwa kutoa msaada kwa ajili ya mpango wa Beyond Zero, hasa utoaji wa vifaa vya ofisi.
"Nina furaha kuwa nilikutana na kuandaa majadiliano na Balozi wa China nchini Kenya Wu Peng katika Ikulu, ambaye alinihakikishia kujitolea kwa serikali yake kuendelea kuunga mkono jitihada hizo za Beyond Zero wakati tunapoungana pamoja kuboresha huduma za afya kwa Wakenya wote kote nchini." Alisema
Mama wa taifa alitoa mfano wa Beyond Zero Medical Safaris, ambayo ni programu ya utoaji wa huduma za matibabu ya bure kwa jamii katika mazingira magumu kwenye maeneo ambayo ni vigumu kufikia, kama mfano wa mbinu ya ubunifu katika kukuza majibu bora kwa magonjwa na changamoto za kiafya.
"Huduma hizi zinawalenga wanawake, watoto na watu wanaoishi na ulemavu, wazee na vijana. Hadi sasa, Beyond Zero Medical Safaris imetoa msaada kwa zaidi ya watu 20,000 na tuna mpango kufikia wengi zaidi mwaka ujao,"alisema.
Akidokeza tu baadhi ya mafanikio ya mpango huo wa afya, mama wa taifa alisema mpango wa kipekee wa mara kwa mara wa uhamasishaji wa rasilimali kupitia mbio za marathon umechangisha fedha za kununua kliniki za kutamba 52 ambazo zimeongeza upatikanaji wa huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi ya ukimwi kote nchini.
Bi Kenyatta alisema kwamba mpango wa Beyond Zero pia unalenga kusaidia juhudi za serikali za kaunti kuimarisha matibabu kwa kuleta huduma za afya karibu na watu maskini na wale wasiobahatika katika jamii.
Kwa muda sasa, mama wa taifa amekuwa akiandaa mbio za kampeni ya Beyond Zero ili kuchangisha fedha za kusaidia shughuli za matibabu kote nchini.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |