Na Majaliwa Christopher
KAMPUNI ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE), East Africa Limited inayotekeleza miradi mbalimbali nchini Tanzania imekanusha madai kuwa kazi zake zimekuwa zikitekelezwa chini ya viwango.
"Hivi karibuni imerepotiwa kuwa baadhi ya shule zilizojengwa na baadhi ya kampuni za China ikiwemo CRJE zimejengwa chini ya viwango na ziko kwenye hali mbaya.
CRJE inapenda kuuelezea umma wa Tanzania na vyombo vya habari kwamba miradi yote inayotekeleza ni kwa mujibu wa makubaliano na viwango vilivyowekwa," taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na kampuni hiyo jana Julai 9, 2019 alisema.
Taarifa iliyosainiwa na Afisa Rasilimali Watu wa CRJE—Ofisi ya Zanzibar, Bw. Yussuf Fabian Simon ilisema kuwa kazi zote zilizowahi kutekelezwa na kampuni hiyo visiwani humo vinakidi viwango na kila wanapokamilisha mradi wowote wanakabidhiwa cheti.
"CRJE siku zote inafanya kazi kwa ushirikiano na mwajiri na inabeba pia majukumu ya kusimamia merekebisho kwa mujibu wa mkataba husika," sehemu ya taarifa hiyo ilisisitiza.
Kampuni hiyo iliongeza kuwa huwa inafanya kazi zake kwa kufuata viwango vya kimataifa na si vinginevyo
"Kampuni ya CRJE iko hapa kufanya kazi na serikali ya Zanzibar pamoja na sekta binafsi kuhakikisha miradi mingi ya kimaendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa ubora unaostahili,' Bw. Simon alisema katika taarifa hiyo.
Iliongeza kuwa, CREJ imwawahi kushinda tuzo mbalimbali za ubora nchini Tanzania, ikiwemo ya mwaka 2008 iliyotolewa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi.
Tuzo zingine ilizowahi kushinda ni pamoja na kuwa kampuni bora ya nje inayosaidia ukuaji wa viwanda vya ndani ya mwaka 2011 iliyotolewa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi pamoja na cheti ya Shukrani kutambua ushiriki wake kwenye uokoaji katika tukio la ajali ya boti ya MV Skagit iliyotokea Julai 18, 2012 katika Bahari ya Hindi.
Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na CRJE Zanzibar ni pamoja na hoteli ya nyota tano ya Kiwengwa iliyokamilishwa mwaka 2005 hoteli ya Kizimkazi iliyokamilika mwaka 2011, hoteli ya Park-Hyatt pamoja na miradi mingine ya serikali ikiwemo jengo la Bodi ya Mapato Zanzibar
Kampuni hiyo ya ujenzi kutoka China ilitoa taarifa hiyo siku chache baada ya baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi --Zanzibar kudai kuwa makampuni ya nje ya ujenzi yanayotekeleza miradi mbalimbali visiwani humo yamekuwa yakifanya kazi chini ya viwango vya kimataifa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |