• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Vyuo vya China, Tanzania Kushirikiana programu ya uhandisi wa ndege

    (GMT+08:00) 2019-07-15 09:53:06

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    CHUO cha Usafirishaji nchini Tanzania (NIT) na Zhengzhou University of Aeronautics (ZUA) cha China vimepanga kushirikiana kufundisha programu ya uhandisi wa ndege.

    Hatua hiyo itasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa wataalamu katika sekta ya usafiri wa anga katika nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki ambayo kwa sasa Serikali yake inatekeleza mpango wake wa kufufua Shirika lake la ndege, ATCL.

    Vyuo hivyo viwili vimetangaza siku ya Jumamosi, Julai 13 jijini Dar es Salaam, Tanzania, kuwa wako katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji wa mpango huo.

    Tayari hati ya makubaliano ya utekelezaji wa programu iyo ilikwisha sainiwa hapo mwaka jana. Pamoja na mambo mengine, hati hiyo ya makubaliano inaelezea namna ambayo taasisi hizo mbili za taaluma zitashirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili.

    Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha NIT, Prof Zacharia Mganilwa, umuhimu wa kuanzishwa kwa programu hiyo kwa ushirikiano kati yake na chuo hicho cha China umekuja baada ya kufufuliwa kwa Shirika la Ndege Tanzania huku wataalam katika sekta hiyo wakiwa hawatoshi.

    Kwa mujibu wa takwimu, hadi mwaka 2016, Tanzania ilikuwa na wataalam 74 tu wa ndege huku mahitaji yakiwa ni 236.

    Kwenye programu hiyo, wanafunzi katika fani hiyo ya uhandisi wa ndege watakuwa wanasoma miaka minne ambapo miwili watakuwa wakisoma Tanzania na miaka mingine miwili wanamalizia nchini China.

    "Wanafunzi watadahiliwa katika chuo cha Usafirishaji Tanzania ambapo watasoma kwa miaka miwili na baadae kwenda kumalizia miaka miwili iliyobaki katika chuo cha ZUA nchini China," alisema Prof Mganilwa.

    Waatalam kutoka hizo taasisi mbili, walikutana kujadiliana namna bora ya kutekeleza hati ya makubaliano waliosaini mwaka jana.

    "Programu hii pia itasaidia kuchochea na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu --China na Tanzania," aliongeza mkuu huyo wa Chuo.

    Kiongozi wa ujumbe huo kutoka chuo cha ZUA, Bw. Fu Qiang alisema ushirikiano huo kati ya vyuo hivyo viwili utazidi kuimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

    "Chuo cha ZUA kilianzishwa mwaka 1949 na kwa sasa kina jumla ya wanafunzi wapatao 20,000. Baada ya kusainiwa kwa hati hiyo ya makubaliano tumekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha makubaliano yote yanatekelezwa kadri ya muda uliowekwa," alisema Bw. Fu.

    Mwaka 2017, aliyekuwa Balozi wa China nchini Tanzania Dr Dk. Lu Younging alitangaza kuwa China kwa kushirikiana na Tanzania zilikuwa zinatarajia kujenga chuo kikubwa zaidi cha usafirishaji nchini Tanzania kwa gharama za Dola za Marekani milioni 62 sawa na Shilingi Bilioni 138.3 za Tanzania.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako