Na Majaliwa Christopher
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa mchango wake katika kuboresha sekta ya afya visiwani humo.
Akiagana na timu ya wataalam wa afya kutoka nchi hiyo ya Asia ya Mashariki jana Jumamosi, Julai 13, Waziri wa Afya wa Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed, alisema China imekuwa ikituma timu ya madaktari kila mwaka kusaidia kutoa huduma za afya katika hospitali mbalimbali Zanzibar.
Timu ya wataalam hao walioagwa mwisho wa wiki walikuwa Zanzibar kwa muda wa mwaka mmoja, huku Waziri Mohamed akisisitiza utayari wa Serikali hizo mbili kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo.
"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Mohamed Shein imepata maendeleo makubwa sana katika kuboresha sekta ya afya. Lakini, hata hivyo, bado inahitaji msaada kutoka kwa wadau wa maendeleo kama China ili kuboresha zaidi huduma za afya katika maeneo yote," alisema Bw. Mohamed.
Kwa kutambua mchango wa wataalamu hao kutoka China katika kutoa huduma za afya visiwani humo, Waziri Mohamed, kwa niaba ya Serikali aliwatunuku madaktari hao vyeti na medali.
"Napenda kuwapongeza madaktari waliomaliza muda wao kutoka nchini China. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Zanzibar wanathamini sana huduma zinazotolewa na madaktari hawa pamoja na mafunzo wanayoyatoa kwa madaktari Wazalendo," aliongeza Bw. Mohamed.
Mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ilianza kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kwa kuleta madaktari kutoka nchini humo.
Hadi sasa China imekuwa ikiendelea na utamaduni wake huo ambao unatokana na historia kubwa iliyopo kati ya China na Zanzibar ambayo imeanza tokea karne nyingi zilizopita.
Hata hivyo, mbali ya masirikiano inayotoa katika kuimarisha sekta ya afya, Serikali ya Watu wa China imeweza kusaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya kilimo, viwanda, michezo, habari na mawasiliano ujenzi na nyinginezo.
Waziri Mohamed pia aliishukuru Serikali ya Watu wa China kwa misaada yake ya kujenga na kuboresha hospitali ikiwemo ile ya Abdalla-Mzee iliyopo Pemba.
Balozi Mdogo wa China, visiwani Zanzibar Bw. Xie Xiaowu alisema sekta ya afya ni moja ya vipaumbele vyake katika ushirikiano wake na Serikali ya Zanzibar.
Kiongozi wa timu hiyo ya wataalamu waliondoka Zanzibar kurudi China mwisho wa wiki, Bw. Zhang Zhen alisema licha ya changamoto ndogondogo zilizojitokeza katika kipindi chote walichokuwa Zanzibar, walifanikiwa kushirkiana na madaktari wazalendo katika kutoa huduma za afya katika vituo mbalimbali.
"Licha ya changamoto ndogondogo, tulifurahi sana kuwa hapa Zanzibar. Watu wa hapa ni wakarimu na wanapenda sana watu. Hali hii ilitusaidia kuwahudumia watu wengi kwa ufanisi mkubwa," alisema Bw. Zhang.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |