• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Hospitali ya Shandong, JKCI ya Tanzania kushirikiana matibabu ya moyo

    (GMT+08:00) 2019-07-29 10:05:37

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    CHINA na Tanzania, siku ya Ijumaa, Julai 26, 2019 jijini Dar es Salaam, zimetiliana saini ya makubaliano ya ushirikiano katika nyanja ya upasuaji na matibabu ya moyo.

    Ushirikiano huo utawezesha kuwepo kwa kambi ya upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na yataratibiwa kwa ushirikiano kati ya madaktari wa taasisi hiyo na wa jimbo la Shandong ya nchini China.

    Hati ya makubaliano ilisainiwa kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya JKCI, Prof Mohamed Janabi na Makamu wa Rais Hospitali ya Jimbo kuu la Shandong, China, Bw. Li Lepin.

    Tukio hilo lenye lengo la kuboresha huduma za matibabu ya moyo katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki lilishuhudiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Bi. Ummy Mwalimu na Naibu Waziri wa Afya wa China Bw. Li Bin.

    Akizungumza baada ya kutiliana saini, Bw. Li Alisema makubaliano hayo mapya yaliyotiliwa saini ni utekelezaji wa ahadi alizotoa Rais wa China Xi Jinping katika mkutano wa mwaka jana 2018 wa FOCAC uliofanyika jijini Beijing na kuhudhuriwa na marais kutoka nchi za Afrika.

    Alisema pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo, Rais Xi aliahidi kuimarishwa kwa ushirikiano katika sekta ya afya kati ya China na mataifa ya Afrika.

    Bw. Li alisema kuwa makubaliano hayo pia yanalenga kufanya taasisi hiyo ya moyo kuwa moja ya hospitali kubwa na maarufu katika kutoa huduma za moyo nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.

    "Nimefurahishwa na namna madaktari katika hospitali hii wanavyofanya kazi, ninaamini ushirikiano huu utazidi kuboresha huduma ya matibabu ya moyo hapa nchini Tanzania," alisema Bw. Li.

    Alisema kuwa nchi yake inafurahi kusikia kwamba vifo vinavyotokana na matatizo ya moyo nchini Tanzania vimepungua na vilevile Serikali ya nchi hiyo imepunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya huduma hiyo.

    Kupitia makubaliano hayo, alisema madaktari kutoka China watakuwa wanatembelea taasisi hiyo ya moyo kubadilisha uzoefu na wenzao huku madakatari wa Tanzania pia wakipewa nafasi ya kwenda kujifunza katika hospitali yao ya Shandong.

    "Tutaendelea Kushirikiana pia katika eneo la utafiti. Tunataka kituo hiki (JKCI) kiwe bora na cha mfano katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki," alisema na kusisistiza kuwa ushirikiano wa Tanzania na China ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hizo mbili.

    Kw upande wake Mkurugenzi wa JKCI Prof Janabi alisema taasisi yake itaendelea kutoa huduma bora kwa ajili ya wagonjwa wa ndani na wa nje ya nchi.

    Alisema makubaliano hayo itasaidia hospitali hiyo kupiga hatua zaidi katika utoaji wa huduma nchini Tanzania.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako