Na Majaliwa Christopher
HUKU uhusiano wa kibishara na uwekezaji ukizidi kukukua na kuimarika kati ya Tanzania na China, wafanyabiashara kutoka Mkoani Mtwara, kusini mwa nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki, wanatarajia kutembelea China hivi karibuni ili kujifunza fursa mbalimbali za kibiashara zikiwemo za uwekezaji wa viwanda ili kuendana na kasi ya Tanzania ya viwanda.
Wafanyabiashara hao ambao pia watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka hiyo hiyo ya Asia ya Mashariki ambayo ni pili kwa utajiri duniani, watafadhiliwa na Benki ya NMB --moja ya benki kubwa nchini Tanzania.
Akizungumza na wafanyabiashara Mkoani Mtwara jana Julai 24, 2019, Mkuu wa Kitengo cha Biashara NMB, Bw. Donatus Richard alisema China ni moja ya nchi zenye maendeleo makubwa ya kiuchumi hivyo wafanyabiashara wa Tanzania wana mengi ya kujifunza nchini humo.
"Tumekuwa tukitoa mafunzo mbalimbali kwa wajasiriamali ikiwa ni pamoja na kutunza rekodi, masoko na namna ya kujisajili kibiashara ndio maana tunaamini kuwa wakienda nchini China wakajifunza zaidi wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu na katika safari hiyo tunatarajia kupeleka wafanyabiashara 10" alisema Bw. Richard.
Benki hiyo ya NMB pia imewahamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kuongeza mitaji kwa kukopa, ili kuweza kupiga hatua kiuchumi.
"Ushindani wa kibiashara nchini Tanzania umekuwa mkubwa, nasi ndio maana tunatumia klabu hizi kufundisha mifumo, njia na mipango rafiki ya kuimarisha biashara za wateja wetu hawa ambao pia ni mabalozi wetu kwa jamii. Tutawapeleka China kujiongezea maarifa juu ya hilo," alisema Richard.
Bw. Richard aliongeza kuwa wafanyabiashara hao mbali na fursa wataenda kujifunza Katika nyanja mbalimbali ili kujua namna gani wanaweza kufanya biashara kimataifa.
"Wapo wafanyabiashara walioanza kukopa shilingi milioni mbili lakini leo hii ni mabilionea ukiwaongezea ujuzi na maarifa kwa kuwapa mafunzo mbalimbali na kuwakutanisha na wafanyabiashara mbalimbali wanaweza kuwa chanzo kizuri cha kuinua uchumi wa taifa letu" alisema Bw. Richard.
Mfanyabiashara kutoka Mtwara, Bw. Milton Christopher, alisema zipo nafasi nyingi za wafanyabiashara zinazoweza kuwanufaisha, ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kwuanufaisha.
"Unajua endapo wafanyabiashara wataangalia ukuaji wa uchumi, kwa namna ya kukuza uchumi, nchi inaeza kupiga hatua kubwa ambazo zinaweza kuongeza kasi ya uzalishaji mali," alisema Bw. Christopher.
Ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya China na Tanzania unaendelea kukua kwa kasi ikihusisha wafanyabishara wa nchi hizo mbili kutembeleana kusaka fursa mbalimbali na kubadilishana uzoefu.
Hivi karibuni, kati ya Julai 20 na 23, wafanyabiashara 25, kutoka Kampuni 15 za Jimbo la Zhejiang China, walifanya ya ziara ya siku tatu nchini Tanzania kusaka fursa za biashara.
Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kukutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali kuhusu fursa za biashara na uwekezaji zilizopo Tanzania na ililenga kukuza mahusiano ya kiuchumi baina ya Jimbo la Zhejiang na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo kama vile teknolojia, mawasiliano, ujenzi na uchukuzi, afya na madini.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |