Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM
Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wamefanya mkutano na wafanyabiashara toka China kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji nchini pamoja na sheria ya kazi na ajira pamoja na kujadili changamoto za kibiashara wanazokutana katika uwekezaji wao.
Mkutano huo ulioshirikisha ATE na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China nchini Tanzania pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la Norway (NHO).
Mkurugenzi Mtendaji wa ATE Dk. Aggrey Mlimuka anasema ATE wamekuwa wakiandaa mikutano kama hiyo mara kwa mara kujadili na kutoa elimu kuhusu sheria za Kazi na Ajira nchini ikiwa ni moja ya juhudi za kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wawekezaji wa kutoka China ili kuongeza uzalishaji na ushindani wa kibiashara.
"Kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengine hapa nchini, Jumuiya wa Wafanyabiashara wa Kutoka China bado wameendelea kukumbana na changamoto nyingi zinazohusiana na Uwekezaji, Masuala ya Kodi, utekelezaji wa sheria za kazi na Ajira, Ajira za wafanyakazi, mikataba, Taratibu za Usitishwaji wa mikataba, Masaa ya kazi, Likizo, Vibali vya Kufanya kazi kwa Wageni," amesema Dkt Mlimuka.
Amesema changamoto nyingine nyingi zinaendana na hivyo ATE kwa kushirikiana na wadau wao wameona ni vyema kuandaa mkutano huo ili kuweza kujadili na kutafuta ufumbuzi wa Changamoto hizo.
Dkt. Mlimuka pia alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi wa Taifa letu.
Mkutano huu wa ngazi ya juu umejumuisha wadau mbalimbali kutoka Kituo cha Taifa cha Uwekezaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Kamshna wa Kazi na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |