Theopista Nsazugwanko, DAR ES SALAAM
SEKTA ya utalii nchini Tanzania inazidi kukua baada ya kupokea watalii 120 kutoka Hong kong, China kuwasili nchini kwa ajili ya kutembelea hifadhi mbalimbali za Taifa na maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii nchini.
Watalii hao waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) mkoani Kilimanjaro na kupokelewa na watendaji mbalimbali katika sekta hiyo inayoelezwa kukua kwa asilimia 13.5 katika mwaka mmoja uliopita.
Viongozi mbalimbali waliwakaribisha watalii hao akiwamo Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) jaji Thomas Mihayo na Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Bibi Devotha Mdachi.
Akizungumza wakati wa mapokezi hao,Jaji Mihayo anasema kuongezeka kwa watalii nchini inatokana na juhudi na mikakati ya bodi hiyo na wadau wengine pamoja na maafisa wa bodi na kusaidia kuongeza mapato ya serikali.
Huku Bibi Mdachi anabainisha kuwa wameweka mikakati kutangaza vivutio vya utalii nchini katika nchi za Mashariki ya mbali,Mashariki ya kati,Ulaya ,Marekani na Asia kwa kushirikiana na maafisa wa balozi za Tanzania katika nchi husika.
Anasema wakiwa nchini watalii hao watatembelea Hifadhi za Taifa za Serengeti na Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro kujionea majabu ya dunia ambapo kwa mujibu wa ripoti ya utalii ya kimataifa mwaka jana idadi ya watalii nchini imeongezeka mpaka milioni 1.5 mwisho wa mwaka jana ukilinganisha na milioni 1.3 mwaka 2017.
Naibu Waziri Kanyasu amebainisha kuwa wizara imeridhishwa na mikakati ya kuongeza watalii inavyoendelea kuleta watalii kutoka maeneo mbalimbali hususan China.
Watalii hao wiki hii wanatarajia kuhudhuria mkutano wa biashara jijini Arusha watakutana na wafanyabiashara wenzao wa Tanzania na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya uwekezaji katika nyanja tofauti.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |