• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Balozi wa China nchini Tanzania ataka taasisi za Confucius kufundisha Kiswahili

    (GMT+08:00) 2019-08-22 10:26:15

    Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM

    LUGHA ni muhimu katika mawasiliano ikiwemo kubadilishana tamaduni za aina mbalimbali,biashara,utalii na muingiliano wa watu katika dunia hii ambayo kwa sasa imekuwa kama kijiji kwa mtu wa eneo moja kwenda kuishi au kufanya shughuli mbalimbali katika eneo lingine.

    Kutokana na umuhimu wa jamii moja na jingine kujikita katika kufahamu lugha, China na Tanzania nchi zenye uhusiano wa kidiplomasia kwa miaka 55 sasa,imekuwa vema kwa wananchi wake kufahamu lugha zinazotumika katika mataifa hayo kwa raia wa Tanzania kujifunza kichina na Wachina kujifunza kiswahili kwa ajili ya mawasiliano baina yao.

    kutokana na umuhimu wa lugha, China imesaidia vijana wa Tanzania kujifunza lugha ya kichina ili kuelewa nchi hiyo kwa undani na kutoa nafasi ya kuimarisga urafiki kati ya China na Tanzania hivyo kupata uelewa kwa undani kuhusu China.

    Hivyo, tangu mwaka 2013 idara ya ELimu nchini China na Tanzania waliungana na kuanzisha vituo vya utamaduni vya taasisi ya Confucius viwili na madarasa mawaili nchini Tanzania iliyosaidia mpaka sasa takribani shule za msingi,Sekondari na vyuo 50 kufundisha lugha ya Kichina ,Sanaa na tamaduni za nchi hiyo.

    Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke anabainisha kuwa kwa sasa kuna zaidi ya wanafunzi 10,000 wanaosoma lugha ya Kichina nchini Tanzania hivyo kutokana na lugha ya Kiswahili kuenea kwa kasi duniani hususan katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika baada ya Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuitambua rasmi kama lugha rasmi ya nne katika jumuiya hiyo ni dhahiri itaongeza matumizi ya lugha hiyo.

    Wang anaeleza kuwa kiswahili kwa sasa kitatumika katika biashara, utalii, muingiliano wa watupamoja na mikataba kati ya China na Afrika hivyo wanahitajika wataalamu zaidi wa lugha hiyo.

    Alisema nchini China kila mwaka kuna wahitimu takribani 20 wa lugha ya kiswahili, hivyo akataka taasisi ya Confucius na jamii ya Wachina waliopo nchini Tanzania kuwa na madarasa ya Kiswahili kuwezesha wachina kuwasiliana vema na rafiki zao wa Tanzania.

    "Hivyo inahitajika zaidi ufahamu wa lugha ya Kiswahili pia, hivyo nahamasisha vyuovya tamaduni za China hivyo na jamii ya wachina nchini kuanza masomo ya Kiswahili kuwezesha wachina kuwasiliana vema na rafiki zao watanzania" alisema.

    Kiswahili ndani ya SADC Kabla ya Wakuu wa nchi za SADC kupitisha Kiswahili kuwa lugha ya nne ndani ya jumuiya hiyo ikiungana na Kiingereza, Kifaransa na Kireno, Baraza la mawaziri wa SADC lilipitisha mapendekezo 107 ikiwamo kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya nne rasmi katika jumuiya hiyo.

    Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa mkutano wa baraza hilo hivi karibuni, Mwenyekiti wa Baraza hilo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema wameridhia mapendekezo hayo 107.

    Profesa Kabudi akizungumza kuhusu Kiswahili, aliwashukuru wajumbe wa baraza kuona Kiswahili kinafaa kupendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC na hatua hiyo inadhihirisha kuthamini mchango Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

    Akifafanua, Profesa Kabudi alisema Kiswahili kilitumika kama lugha ya ukombozi kwa wapigania uhuru, lakini pia kinatumika kwenye nchi nyingi ikiwemo Somalia, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kaskazini mwa Zambia na inafundishwa kwenye vyuo vikuu 53 duniani. Afrika Kusini inaanza kukifundisha katika shule za msingi na sekondari mwakani.

    Yashika kote Afrika Kwa kuingiza Kiswahili SADC, hii inakuwa lugha ya kwanza ya Afrika kuwa lugha rasmi katika jumuiya za kimataifa, ikiwemo EAC, SADC na Umoja wa Afrika (AU).

    Katika moja ya mikutano ya AU jijini Addis Ababa, Ethiopia, Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli aliweka rekodi ya kuwa Rais wa Kwanza kuhutubia Umoja wa Afrika kwa lugha ya Kiswahili.

    Hayo yalikuwa mapinduzi makubwa kuelekea katika kuitangaza lugha hiyo adhimu duniani. Hizi ni habari njema kwa Watanzania, ambako Kiswahili lugha ya taifa na kwamba Watanzania sasa wanastahili kujivunia na kuvuna matunda ya juhudi za kukikuza Kiswahili.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako