Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Huatan Investment Group Limited ya nchini China siku ya Jumanne, Agosti 27, 2019, imezindua kiwanda cha kuchakata betri za magari zilizotumika nchini Tanzania.
Kiwanda hicho kimezinduliwa katika kijiji cha Nyamwange wilaya ya Rufiji katika mkoa wa Pwani, nchini humo na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Evarist Ndikilo.
Mkurugenzi wa Huatan Investment Group Limited Bw. Xian Ding alibainisha kuwa kiwanda hicho kinatarajiwa kuchakata betri zilizotumika tani 10,000 na kitatoa ajira za moja kwa moja 60 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 200.
"Kwa kuanza tutakuwa tukisafirisha malighafi kwenda nje ya nchi zinazotokana na betri zilizochakatwa kwa ajili ya kutengeneza betri mpya."
"Lakini baada ya mwaka mmoja mpaka miwili ijayo kulingana na ustawi wa biashara tutaanza kwa kuchakata na kutengeneza betri Tanzania kwa ajili ya soko la ndani," alisema Ding.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bw. Evarist Ndikilo aliwataka wananchi kushirikiana na wawekezaji ili kuwa mabalozi wa kuvutia uwekezaji nchini.
"Tukiwapa ushirikiano wawekezaji wetu wataleta wengine. Tuwe na matumizi bora ya ardhi, mkulima akae eneo lake na mfugaji akae eneo lake."
"Maeneo ya wawekezaji nayo tuyaache wakija kuwekeza msiwauzie kwa bei ya kuwaumiza iwe ina manufaa kwa pande zote," amesema.
Amebainisha kuwa kuna wawekezaji kutoka Uarabuni wanataka kuwekeza katika kiwanda cha sukari kitakachotoa ajira kwa watu wengi zaidi.
Meneja wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) kanda ya Mashariki Bw. Venance Mashiba amesema uwekezaji huo ulipitia katika kituo hicho mwaka 2017 na gharama ya uwezeshaji ilitajwa kuwa ni Dola 630,000 za Marekani.
Ushirikiano wa Tanzania na China umeendelea kukua kwa kasi hususan katika masuala ya kiuchumi na kwamba, miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa na mingine inaendelea.
Uwekezaji wa China nchini umekua mara kumi kutoka Tsh1.58 trilioni hadi Tsh15.82 trilioni katika kipindi cha miaka sita.
Hali hiyo inatokana na kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo ambazo zimekuwa na urafiki muda mrefu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |