Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi (OR) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi "Gavu" amesema uamuzi wa Serikali wa kuwaomba washirika wa maendeleo kutoka China kufanya mafunzo ya Upishi na Ukarimu hapa Zanzibar, kunatoa fursa ya kutekeleza matakwa ya kisheria na kanuni za Utumishi wa Umma.
Waziri Gavu amesema hayo katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul wakil katika ufunguzi wa mafunzo ya Upishi na Ukarimu, yanayoendeshwa na Wakufunzi kutoka nchini China. Mafunzo hayo yanayowashirikisha watumishi 45, yatadumu kwa kipindi cha wiki nne, yakiwa na lengo la kuwaongezea ufanisi, uwajibika na kuleta tija katika utumishi wa umma.
Akizungumza na washiriki wa amafunzo hayo, Gavu alisema mafunzo ya watumishi wa umma ni jambo lililotiliwa mkazo katika sheria ya utumishi wa umma Namba 2 ya mwaka 2011 pamoja na kanuni za utumishi wa Umma za mwaka 2014. Alisema uamuzi wa serikali kuomba kufanyika mafunzo hayo hapa nchini unalenga kuwapa fursa watumishi wengin zaidi kupata mafunzo hayo muhimu kwa vitendo katika mazingira wanayofanyia kazi.
"Napenda kukusitizeni ndugu washirki wa mafunzo kuiunga mkono na kuthamini dhamira njema ya mheshimiwa Rais ya kuhakikisha watumishi wa umma wanapatiwa mafunzo ya mda mrefu na mda mfupi", alisema.
Alisema kutokana na mafunzo hayo, nchi itaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo na kuimarika kwa ustawi wa wananchi wake. Aliwataka washirki wa mafunzo hayo kudumisha nidhamu katika kipindi chote cha masomona kujenga mashirkiano na wakufunzi hao pamoja na kubeba dhima ya kuwa walimu kwa watumishi wengine waliokosa fursa hiyo.
Alisema mafunzo hayo sio tu kuwa yatawanufaisha watumishi na kupata maarifa mapya katika kuwahudumia Viongozi wakuu na vitengo maalum, lakini pia yatachangia dhamira ya kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Aidha, alsiema hatua hiyo itawapa fursa wakufunzi hao kutoka China kuyafahamu vyema mazingira ya Zanzibar na kupata fursa ya kujifunza mila, silka na utamaduni pamoja na kuona vivutio mbali mbali vya Utalii.
"Tunategemea wenzetu watakapoondoka watakuwa Mabalozi wazuri wa kutangaza Utajiri wa vivutio vya Utalii tulivyonavyo huko nchini kwao, hivyo kuimarisha sekta ya utalii, ikizingatiwa China ni eneo jipya tunalotarajia kupokea watalii", alisema.
Waziri Gavu alipongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, sambamba na hatua ya Taifa hilo kusaidia katika uimarishaji wa sekta mbali mbali za maendeleo na ukuaji wa uchumi. Aliishikuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China pamoja na Taasisi ya 'China National Reseach Institute of Food and Fermentation Industries Corporation Limited kwa kufanikisha mafunzo hayo.
Aidha, alitowa shukurani kwa uongozi wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali, Taasisi ya Maendeleo ya Utalii na Hoteli ya Verde kwa ushirkiano na kufanikisha utoaji wa mafunzo hayo.
Mapema, Balozi mdogo wa China aliopo Zanzibar, Xie Xiaowu alisema mafunzo hayo yatawawezesha kuwajengea uwezo washirki, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii. Vile vile aliipongeza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mashirikiano makubwa yaliowezesha kufanikisha kufanyika kwa mafunzo hayo, hivyo kupanua wigo wa uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya China na Zanzibar.
Nae, Makamu Mkuu wa taasisi ya China National Reseacher Institute of Food and Fermentation Indusries Corporation Limited, Dong Weihong alisema hii ni mara ya tatu kw ataasisi hiyo kuendesha mafunzo hayo, chini ya ushirikiano w akaribu na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Alisema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uwezo katika utoaji wa huduma, hatua iliyobainisha itawezesha kukuza viwango vya maisha ya wananchi, kuitangaza Zanzibar, sambamba na kukuza sekta ya Utalii. Aidha, alionyesha matumaini makubwa aliyonayo kutokana na na mafunzo hayo kuleta tija kubwa kwa washiriki.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |