• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Watanzania waliosoma China waazimia kuvutia wawekezaji

    (GMT+08:00) 2019-10-23 14:36:41

    Majaliwa Christopher

    JUMUIYA ya Watanzania waliosoma China (CAAT) hivi karibuni kiliazimia kuwa kiunganishi kati ya Tanzania na China -- kushawishi wawekezaji kutoka nchi hiyo ya Asia ya Mashariki kuwekeza Tanzania.

    Maazimio hayo yanayolenga kukuza uchumi na kufaidisha nchi hizo mbili yanalenga pia kuendeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli ya kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025.

    China, nchi ya pili kwa utajiri duniani, inaongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania na kwa mujibu wa takwimu, nchi hiyo ya Asia ya Mashariki inabakia kuwa mbia mkubwa wa Tanzania katika uwekezaji na biashara ambapo mwaka jana biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia Dola za Kimarekani Bilioni 3.974.

    Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa mwaka jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Liggyle Vumilia alisema kazi kubwa na ya msingi ya CAAT, wanachama wake na watu waliowahi kuishi nchini China, ni kuunganisha Watanzania na fursa za uwekezaji zilizoko nchini humo ili kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano kwa ujumla katika nyanja mbalimbali.

    Mkutano huo pia uliwawezesha wataalamu wa Tanzania waliosoma China kujadili fursa za biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo.

    "Fursa za biashara kati ya Tanzania na China ni nyingi, hivyo ni jukumu letu kutumia elimu na maarifa tuliyopata katika kuainisha fursa na kuzifanyia kazi ili kujijenga kiuchumi, na kupunguza tatizo la ajira.

    "Nafasi tuliyonayo kama wasomi ni kuchochea maendeleo ya nchi kwa kuleta uzoefu, maarifa na teknolojia kutoka katika mataifa ya nje ili visaidie kujenga uchumi wa viwanda na kuifanya nchi kupiga hatua kimaendeleo," alisema Vumilia.

    Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke, aliipongeza jumuiya hiyo kwa kuendeleza ushirikiano ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Mwenyekiti Mao ze Dong na kuisihi jumuiya iendelee kutumia fursa zilizopo ili kuzinufaisha nchi mbili hizo.

    "Hili ni tukio muhimu kwa pande zote mbili, kwani uwepo wa CAAT utazidi kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili, na jambo muhimu zaidi ni kuendelea kutumia fursa zilizopo katika kutatua changamoto zilizopo," alisema Wang.

    Alisema nchi yake inachukua iko tayari na inafanya kila linalowezekana kunakikisha kuwa uhusiano wake na Tanzania ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 55 sasa unaimarika kwa faida ya wananchi wa Tanzania na China.

    Balozi mstaafu wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali mstaafu Abdulrahman Shimbo, alisema jumuiya hiyo iko katika nafasi nzuri ya kudumisha urafiki wa kihistoria kati ya Tanzania na China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako