Majaliwa Christopher
MAKAMPUNI kutoka China yametekeleza miradi ya ujenzi nchini Tanzania yenye jumla ya Dola za Kimarekani Bilioni 17 (zaidi ya Shilingi Trilioni 39 za Tanzania) na kufanya nchi hiyo ya Asia ya Mashariki kushika nafasi ya kwanza katika kutekeleza miradi ya ujenzi nchini humo.
Mkurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China anayeshughulikia masuala ya Afrika, Bw. Zhang Bin alibainisha haya hivi karubuni jijini Beijing alipokutana na wanahabari waandamizi kutoka nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki -- na kuongeza kuwa miradi mingine zaidi inaendelea kutekelezwa nchini humo na makumpuni kutoka China.
Aliongeza kuwa, wawekezaji kutoka China waliweza pia kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania yenye jumla ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.77, na kufanya nchi hiyo pia kuwa mbia namba moja wa uwekezaji katika nchi hiyo.
Bw. Zhang alibainisha kuwa sekta ya utalii pia ni moja ya maeneo ambayo Tanzania itaanza kufaidika nayo kwa kiasi kikubwa kwani watalii kutoka China wameanza kutembelea nchi hiyo kuangalia vivutio mbalimbali ikiwemo mbuga za wanyama, fukwe za bahari pamoja na milima.
"Kwa sasa watalii kutoka China wanafurika jijini Dar es Salaam, kutembelea fukwe za bahari, visiwa vya Zanzibar na Mbuga ya Wanyama ya Serengeti. Kadri tunavyosonga mbele ndivyo watalii wengi zaidi wanategemewa kutembelea Tanzania ikiwa ni pamoja na kutembelea mji mkuu mpya wa Serikali, Dodoma. Lakini pia habari njema ni kwamba Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) inatarajia kuanza safari za Dar es Salaam-Guangzhou, tunasubiri hii kwa hamu kubwa," alisema Bw. Zhang
Katika sekta ya elimu, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa China imekuwa ikitoa udhamini kwa wanafunzi wa Tanzania pamoja na mafunzo mbalimbali kwa watumishi wa umma, akisisitiza kuwa watazidi kutoa nafasi nyingi zaidi ili kuendeleza ushirikiano katika nyanja hiyo kwa faida ya pande zote mbili.
"Kwa sasa, kuna wanafunzi zaidi ya 5,000 kutoka nchini Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali vya China na pia wataalamu na watumishi wa umma kadha wa kadha wanatembelea China kwa ziara za mafunzo za muda mfupi," alisema Bw. Zhang.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huo, uhusiano katika ya China na Tanzania ambao umedumu kwa takribani miaka 55 sasa, unazidi kuimarika na umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi hizo mbili.
"Tumekuwa na mafanikio makubwa sana kwa kipindi hicho chote, pia, China inaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha inafikia dira yake ya 2025 ya kuwa na uchumi wa kati," alisisitiza.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |