Na Theopista Nsanzugwanko
DAR ES SALAAM
UJUMBE kutoka China ukishirikisha wawekezaji na maofisa wa serikali uMEwasili mkoani Pwani kusaka maeneo ya uwekezaji huku wakitembelea maonesho ya viwanda yanayoendelea mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alieleza kuwa ugenzi huo ni kutoka jimbo la Jebei, China na kuwa muhimu kwani jimbo hilo lina viwanda vingi hivyo kuwezesha pwani kupata wawekezaji.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, Jimbo la Hebei lililopo kaskazini mwa China ndilo lenye viwanda vingi baada ya sehemu kubwa ya viwanda vilivyokuwa Beijing kuhamishiwa huko.
Alisema ujumbe huo unaohusisha maofisa wawili kutoka serikalini na watatu ni wawekezaji, ulialikwa na mkoa na baada ya kutembelea maonesho, utafanya mazungumzo na viongozi wa serikali wa mkoa.
Ndikilo alitaka sekretarieti ya mkoa kuhakikisha wageni hao wanapitishwa kwenye taasisi zinazohusika na uwezeshaji wa wawekezaji.
Aliagiza ugeni huo utembezwe pia kwenye mabanda yanayoonesha maeneo ya uwekezaji wafahamu kwamba ipo ardhi ya kutosha mkoani Pwani.
Wakati huo huo, Ndikilo ameagiza Sekretarieti ya Mkoa kuhakikisha Mwongozo wa Uwekezaji wa Pwani unasambazwa kwenye tovuti na balozi za Tanzania kwenye nchi mbalimbali kwa lengo la kuvutia wawekezaji zaidi.
"Wekeni kwenye tovuti ya mkoa, ya Taifa, kwenye instagram...mwongozo usiishie kwenye makabrasha. Tunataka kuona matokeo chanya," alisema na kuagiza yafanyike mawasiliano na Wizara ya Nje, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iwezeshe nakala kufika kwenye balozi.
Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Pwani ulizinduliwa mwishoni mwa wiki na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye kongamano la fursa za uwekezaji lililofanyika Kibaha kwa uratibu wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).
Umeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP).
Mkurugenzi wa ESRF, Dk Tausi Kida alisema mwongozo umeainisha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizomo mkoani Pwani ambazo zikitumika vizuri zitaboresha maisha ya watu. Fursa hizo ni viwanda, kilimo, utalii, ufugaji, uvuvi na huduma za jamii.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |