Na Majaliwa Christopher
RAIS wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameihakikishia Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuwa sera za nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki kuhusu China hazijabadilika.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Jumatano, Oktoba 23, 2019, Rais Magufuli alimueleza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Kikomunisti (CPC), Bw. Guo Yezhou, kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika jitihada mbalimbali za maendeleo.
Naibu Waziri huyo alimtembelea Rais Magufuli Ikulu na kufanya mazungumzo juu ya mambo mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na China.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke.
Aidha, Dkt. Magufuli alimshukuru Bw. Guo kwa kutembelea Tanzania kwa mara ya pili na pia aliishukuru China kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri na Tanzania.
Aliongeza kuwa Chama cha CPC na Serikali ya China zina mchango mkubwa katika mambo mbalimbali ya Maendeleo nchini Tanzania ikiwemo mchango mkubwa wa chama hicho ambacho kinajenga Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere.
Chuo hicho kinajengwa katika Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uongozi kwa nchi 6 zenye vyama vya ukombozi vilivyoshirikiana na CPC.
Nchi hizo na vyama vyao kwenye mabano ni Tanzania (CCM), Afrika Kusini (ANC), Zimbabwe (ZANU-PF), Msumbiji (FRELIMO), Angola (MPLA) na Namibia (SWAPO).
Rais Magufuli pia alimuomba kiongozi huyo kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China na Mwenyekiti wa CPC Bw. Xi Jinping kwa kutoa tuzo kwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Dkt. Salim Ahmed Salim ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuiwezesha China kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Mapema mwezi huu, Rais Xi alimtunuku Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Dkt. Nishani ya Juu ya Urafiki. Hafla hiyo ilifanyika jijini Beijing katika ukumbi wa Great Hall of the People. Nishani hiyo ilipokelewa na Bi. Maryam Salim ambaye ni mtoto wa Waziri mkuu huyo mstaafu.
Nishani ya Juu ya Urafiki ya Taifa la China ilitolewa kwa Dkt. Salim kutokana na mchango wake wa kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |