Na Theopista Nsanzugwanko
DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema Tanzania itaendelea kuthamini mchango unaotolewa na Jamhuri ya Watu wa China huku akisisitiza kuwa masuala yanayoendelea hivi sasa ambapo Hong Kong inataka kujitenga, yanapaswa kushughulikiwa na China yenyewe.
Balozi Mahiga aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka mitano ya nchi wanachama wa Shirika la Mashauriano ya Sheria za Kimataifa kwa Nchi za Afrika na Asia (AALCO).
Alisema wakati huu ambao Tanzania inazidi kupiga hatua mbalimbali za kimaendeleo, China imekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha baadhi ya maeneo ikiwamo sekta ya ujenzi wa miundombinu pamoja na elimu, suala alilosema linazidi kuchagiza ushirikiano wa muda mrefu baina ya mataifa hayo.
Mbali na hilo, alisema ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na China kwa kiasi kikubwa pia umewezesha kuwepo wa programu za kubadilishana wataalamu katika nyanja mbalimbali zikiwamo kada za afya, elimu na maeneo mengine ya kibiashara na utamaduni ambazo kimsingi zimekuwa na manufaa kwa mataifa yote mawili.
Akizungumzia maadhimisho ya miaka mitano ya AALCO, Balozi Mahiga aliipongeza China kwa kufadhili mkutano huo uliosaidia mafunzo kwa watu wa kada mbalimbali wakiwamo viongozi na wanafunzi katika mataifa zaidi ya 40 kutoka Afrika na Asia na hivyo kusaidia kuleta tija.
Awali, Balozi wa China nchini, Wang Ke pamoja na kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake na Taifa hilo pamoja na msimamo wake juu ya suala lake na Hong Kong, alisisitiza kuwa Hong Kong ni China na kwamba hawapo tayari kuruhusu nguvu za mataifa mengine kuingilia suala la Hong Kong.
Alisema matumaini ya China ni kuona mataifa mengine yanaiunga mkono China katika kusimamia sheria za kimataifa bila kuingilia masuala ya nchi zingine kama ambavyo sheria hizo za kimataifa zinavyoeleza.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |