Na Majaliwa Christopher
RAIS wa Tanzania Dkt. John Magufuli Jumamosi, Desemba 7, 2019, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi linalojengwa na China Civil Engineering Construction Corporation Group na China Railway 15th Bureau Group Co. Ltd za nchini China.
Kampuni mbili hizo za China zinajenga daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3.2 na upana wa mita 28.45 ambalo litakalounganisha mawasiliano ya barabara kati ya Mikoa ya Mwanza na Geita kukatiza Ziwa Victoria.
Rais Magufuli alizitaka kampuni hizo kukamilisha mradi huo unaogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 669 za Tanzania kukamilisha kazi kwa wakati na ikiwezekana hata kabla ya muda. Mradi huo unarajiwa kukamilika mwezi Julai 2023, fedha zote zikiwa zinatolewa na Serikali ya Tanzania
Daraja hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la 6 kwa urefu Barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza, na litajengwa kwa teknolojia ya madaraja marefu inayoitwa Extra Dosed Bridge ambapo litajengwa juu ya nguzo 67 zikiwemo nguzo 3 zenye urefu wa meta 40 na umbali wa meta 160 kutoka nguzo moja hadi nyingine.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Magufuli alowataka wakandarasi wanaojenga daraja hilo-- China Civil Engineering Construction Corporation Group na China Railway 15th Bureau Group Co. Ltd za nchini China. kufanya kazi usiku na mchana ili waweze kumaliza ujenzi kabla ya muda uliopangwa.
Alisema Watanzania wanalihitaji daraja hilo haraka, huku akitoa wito kwa wananchi wa mikoa ya Mwanza na Geita kujitokeza kupata ajira katika kazi za ujenzi, kuuza bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula.
Alisema daraja litasaidia katika utatuzi za kero ya miaka mingi, iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi, na kwamba kukamilika kwake kutakuwa chachu ya kukua kwa uchumi wa kanda hiyo na Tanzania kwa ujumla.
Dkt. Magufuli aliongeza kuwa kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo ni uthibitisho kuwa Tanzania sio masikini na kwamba nchi hiyo ya Afrika Mashariki inaweza, hivyo kutia wito kwa Watanzania wote kutembea kifua mbele kwa kuwa daraja hilo litaharakisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Aloyce Kamwelwe amesema pamoja na ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi, Serikali imejenga madaraja makubwa 77 na madaraja madogo 8,020 na kwamba ujenzi wa madaraja mengine makubwa 6 unaendelea ambayo ni Wami (Pwani), Magara (Manyara), Sukuma (Mwanza), Kitengule (Kagera), Msingi (Singida), Ruhuhu (Ruvuma) na Selander (Dar es Salaam).
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |