Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda, Bugando Medical Centre (BMC) imeokoa Sh. Bilioni moja baada ya kuagiza vifaa tiba, madawa na vitendea kazi kutoka nchini China.
Vifaa hivyo vilivyoagizwa China katika Kontena Sita,zilikuwa zimetengewa sh. Bilioni tatu lakini baada ya kuagiza nchini humo wametumia sh. Bilioni 1.2 pekee.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi alibainisha hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Bugando (Bugando Day) ikiwa ni muda mfupi baada ya kupokea moja ya makontena hayo sita ya vifaa hivyo vilivyogharimu sh. bilioni 1.2 kati ya Sh. bilioni 3 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili hiyo.
Alisema hospitali ya BMC ilikuwa na changamoto ya vifaa tiba na dawa na hivyo kuzua malalamiko kutoka kwa wagonjwa jambo lililousukuma uongozi na menejimenti kutafuta suluhu ya changamoto hiyo ambapo walishindanisha kampuni mbalimbali ili kujua bei ya vifaa tiba na madawa kulingana mahitaji kabla ya kuagiza.
"Ili kupunguza chagamoto hiyo uongozi na menejimenti ya hospitali tulikubaliana kutumia fedha za ndani kuagiza vifaa tiba, madawa, vitendea kazi na sare za watumishi kwa gharama ya sh. bilioni 1.2 kutoka nchini China na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha, endapo tungenunua hapa nyumbani ingetugharimu sh. bilioni 3,"alisema Profesa Makubi.
Alisema kununua madawa na vifaa tiba nje kwa gharama nafuu wameokoa fedha nyingi wanazokusanya na kutumia kidogo lengo likiwa ni kuboresha huduma za tiba kwa wananchi na vitasaidia pia changomoto ya hospitali nyingi za umma kwa sababu zina matatizo ya vifaa tiba.
Dk. Makubi alitaja miongoni mwa vifaa tiba walivyopata kuwa ni mashine 6 za Utra Sound na vifaa vya upasuaji ambavyo vitawezesha wagonjwa kuchunguzwa na kufanyiwa upasuaji kwa haraka zaidi na kupunguza malalamiko ya kuchelewa kuhudumiwa.
Awali Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dk. Fabian Massaga, alisema shilingi bilioni 1.8 kati ya bilioni 3 zilizookolewa kwenye ununuzi wa vifaa tiba na madawa zitatumika kwa maendeleo na kuboresha huduma mbalimbali za hospitali.
Alivitaja baadhi ya vifaa tiba ni vitanda, mashine sita za Utra Sound,vifaa vya upasuaji (operating set), madawa mbalimbali, kompyuta zitakazounganishwa na mfumo na kuondokana na madaktari kutumia majadala kwa ajili ya kumbukumbu za wagonjwa na sare za watumishi vyote vikigharimu sh. bilioni 1.2 fedha za ndani.
Aidha, katika hatua nyingine Profesa Makubi, alisema wanapoadhimisha Siku ya Bugando Day mwaka huu lengo ni kuwakumbusha watumishi wa Hospitali ya BMC majukumu yao, kuonyesha umoja na mshikamano kati yao na watumishi wa Chuo Kikuu Katoliki cha Sayansi za Tiba za Afya (CUHAS).
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha CUHAS, Profesa Paschalis Rugarabamu, alisema wanashirikiana chuo na hospitali kujenga maadili na kuhimiza vijana kutimiza majukumu yao ya utoaji wa huduma za tiba kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma ingawa ni kazi ngumu.
Pia wamepanua wigo wa taaluma nje ya BMC kwa kuwapeleka wanafunzi wa chuo hicho kujifunza kwenye maeneo tofauti licha ya matakwa ya mtaala wanafanya mazoezi katika mazingira halisi kwa kuzijengea uwezo wa elimu na huduma katika hospitali za Sekou Toure na Sengerema DDH.
Hospitali ya Bugando iliyojengwa mwaka 1967 kwa msaada wa Serikali ya Ujerumani Magharibi kwa ushirikiano na Uholanzi kupitia shirika moja la kikatoliki ambapo mwaka huu imeadhimisha miaka 52 na ilifunguliwa, Desemb 3, 1971 na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |