Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kipindi cha miaka tisa imefaidika na misaada mbalimbali ya kuleta maendeleo inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China yenye gharama ya Sh Bilioni 306 iliyosaidia kuleta maendeleo na kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wake.
Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alisema hayo wakati akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wanafunzi waliosoma China katika ngazi mbalimbali.
Alisema kuanzia mwaka 2000 hadi 2019 nchi hiyo imenufaika katika nyanja mbalimbali.
Alisema China ni miongoni mwa nchi za mwanzo duniani kuyatambuwa Mapinduzi ya Zanzibar na hivyo kusaidia harakati za kujenga uchumi na kuleta maendeleo.
Aliongeza kuwa nchi hiyo ilisaidia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa maendeleo ikiwemo kujikita katika sekta ya elimu na ujenzi wa miradi ya viwanda mbalimbali ikiwemo vya kati.
Baadhi ya viwanda vilivyojengwa na nchi hiyo ni kilichokuwa kiwanda cha ngozi na viatu, kiwanda cha sigara, kiwanda cha matrekta kilichoopo Mbweni pamoja na kujenga uwanja wa michezo wa Amaan uliopo Unguja.
"China mara baada ya Mapinduzi ya Januari mwaka 1964 ilitusaidia katika juhudi za kulijenga upya taifa la Zanzibar na ilitusaidia katika miradi ya ujenzi wa viwanda mbalimbali," alisema.
Aidha nchi hiyo tangu mwaka 1965 hadi leo imefanikiwa kuleta madaktari awamu ya 29 na kufika timu ya madaktari 740 waliotoa huduma za matibabu Zanzibar.
"China wamekuwa wakitusaida katika sekta ya sfya kwa kuleta madaktari bingwa tangu mwaka 1965. Sasa wameifanyia ukarabati mkubwa hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo Pemba," alisema.
Aliutaja msaada uliotolewa hivi karibuni na China wa Sh Bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za madaktari na wafanyakazi katika hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo Pemba.
"Kupitia msaada huo tutaimarisha na kufanya ukarabati mkubwa studio za kurushia matangazo za Redio na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ili zifanye kazi zake vizuri kutoa huduma na elimu kwa jamii," alisema.
Akizungumza katika sherehe fupi ya kuwapongeza wafanyakazi waliopata mafunzo mafupi nchini China, Balozi mdogo wa China , Zainzibar Xie Xiaowu alisema tayari nchi hiyo katika kipindi cha miaka minne imetoa nafasi za masomo 126 kwa wanafunzi ngazi ya Shahada ya Kwanza.
Aidha alisema katika kipindi cha miaka minne wanafunzi 700 wamepata nafasi za mafunzo ya kozi fupi nchini China.
"Kwa kifupi idadi ya watu waliopata mafunzo mbalimbali ya ufundi ya kitaalamu kutoka China imeongezeka na kufikia 380," alisema Balozi Xiaowu.
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China iliyatambuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Februari 6, mwaka 1964 na kufunguwa ubalozi mdogo ambao umedumu hadi sasa ukiwa na lengo la kufuatilia kwa karibuni sana misaada inayotolewa na nchi hiyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |