Na Majaliwa Christopher
RAIS wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein Jumatatu, Januari 6, 2019, ameshiriki hafla ya ufunguzi wa shule ya sekondari ya Mwembeshauri iliyojengwa na Kampuni ya Group Six International Limited kutoka China.
Ujenzi was shule hiyo umetekelezwa kwa mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wahisani Opec Fund for International Developement (OFID), kupitia mradi wa Zanzibar Third Education Project (ZATEP).
Shule hiyo iliyojengwa na kampuni hiyo ya China imegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 3.5 za Tanzania --kati ya hizo shilingi Bilioni 3.2 zimetumika kwa shughuli za ujenzi na zaidi ya shilingi Milioni 361.1 ni gharama za ununuzi wa vifaa mbalimbali, zikiwemo komputa na vifaa vya maabara.
Vilevile shule hiyo ina uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 2,560 kupitia mikondo miwili kwa wastani wa wanafunzi 40 kwa darasa.
Katika halfa hiyo, Rais Shein alisema Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, kutokana na misingi bora iliyowekwa na muasisi wa Taifa hilo, marehemu Abeid Amani Karume.
Alisema ukombozi uliofanywa na Chama cha ASP chini ya Uongozi thabiti wa marehemu mzee Abeid Amani Karume mwaka 1964, umeweka misingi bora ya upatikanaji wa elimu nchini, na kubainisha kuwa itaondelea kutolewa bure katika awamu zijazo.
Dkt. Shein alisema katika awamu tofauti za Uongozi, Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuendeleza sekta ya elimu kwa kuimarisha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa skuli hadi kufikia 381 hivi sasa kati yake skuli 284 zikiwa za Sekondari.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kufanya juhudi kubwa kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokwaza maendeleo ya elimu nchini, ikiwemo upatikanaji wa vitabu na madawati, akibainisha awamu ya pili ya uagizaji madawati 42,135 kutoka nchini China kwa ajili ya skuli za msingi.
Rais Dkt. Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea kukimarisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kuongeza vitivo na program mbali mbali za masomo ili kuhakikisha Taifa linapata wataalamu wengi kupitia nyanja tofauti.
Alisema Serikali ya Zanzibar imelipa kipaumbele suala la elimu na kubainisha katika Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 178.9 kwa ajili ya sekta ya elimu nchini.
Aidha, alisema changamoto ya upungufu wa walimu wa Sayansi inafanyiwa kazi ambapo tayari limeanza kupatiwa ufumbuzi kwa msaada wa wahisani mbali mbali.
Katika hatua nyengine, Dkt. Shein alipingana na mitazamao ya baadhi ya watu wanaodai elimu imeshuka nchini, akisema haijulikani kipimo gani kilichotumika kuhusisha ya dhana hiyo, kwa kuzingatia kuwa hivi sasa Zanzibar imekuwa na Vyuo vikuu kadhaa, wakati ambapo zamani havikuwepo.
Alisema weledi wa kuzungumza lugha ya Kiingereza sio kigezo cha kupimwa kiwango cha elimu akibainisha kuwepo nchi kadhaa duniani zilizopiga hatua kubwa za maendeleo ambapo hutumia lugha zao za Taifa katika kufundishia hadi vyuo vikuu.
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alisema ujenzi wa skuli hiyo ya ghorofa mbili una lengo la kuondokana na ufinyu wa nafasi, na kubainisha kuwa zitatumika na wanafunzi wa skuli mbili na kuondokana na kadhia ya mazingira mabaya yaliopo katika skuli za Darajani na Vikokotoni, ambazo zimezungukwa na shughuli za kibiashara.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |