Na Eric Biegon-NAIROBI
Kitabu kitakatifu kinasema "Kila kitu kina majira yake, kila jambo duniani lina wakati wake" ……."wakati wa kutawanya mawe na wakati wa kuyakusanya mawe pamoja. Wakati wa kukumbatia na wakati wa kujizuia kukumbatia ... wakati wa kurarua na wakati wa kushona, wakati wa vita na wakati wa amani."
Kwa mujibu wa mlipuko wa virusi vya korona unaoendelea, msemo huu unanena kweli. Hakika huu si wakati wa kulaumiana au kulimbikiziana makosa. Sio wakati wa kuangalia udhaifu au upungufu wa mtu au taifa. Na ni dhahiri kwamba si wakati wa kunyosheana kidole cha shutuma au kujaribu kuhalalisha janga. Bila shaka huu sio wakati wa kubagua.
Badala yake, ni wakati wa kuja pamoja. Huu ni wakati wa kusonga mbele kwa lengo moja. Lengo hilo ni kupambana na "adui" wa sasa wa binadamu ambayo ni virusi vya korona. Muda umewadia kwa wanadamu wote kuinua sauti kwa pamoja na kutangaza vita dhidi ya janga hili.
Inasikitisha kuona kwamba kiwango fulani cha ubaguzi kimeelekezewa watu wa asili ya Kichina hata ingawa wao wanafanya kila wawezalo kuzuia kuenea duniani kwa ugonjwa huu wa kuambukiza.
Jambo linalohitaji kipaumbele kwa sasa ni janga hili ambalo kwa muda mfupi limesababisha vifo vya watu zaidi ya 500. Na hofu bado ipo kwani maradhi haya yanaenea kwa kasi. Virusi hivi havijui mipaka.
Ni dhahiri, China imejizatiti vilivyo kwa kupambana dhidi ya virusi hivi vya korona. Serikali iliyo na makao yake jijini Beijing, limekuwa na tahadhari sana. Wataalamu wanahoji kuwa isingelikuwa ni juhudi kabambe za China, basi virusi hivyo vingeenea mbali na kwa kasi. Kuna hofu kuwa kiwango cha madhara yake kingekuwa mkubwa mno.
Lakini, iwapo tumejifunza lolote kutoka siku chache zilizopita, basi ni kwamba, sisi kama binadamu tumo kwenye janga hili pamoja na China ambayo inahitaji msaada, bila kujali kiwango, kutoka kwa mataifa mengine duniani.
Kama taifa linalozingatia uwajibikaji, China lilitangaza karantini ya siku 14 kwa watu wote kutoka China bara.
Hospitali za muda katika mji mkuu wa Wuhan zimejengwa kwa wakati wa rekodi. Kumbi za michezo, vituo vya maonyesho na maeneo ya michezo, kwa sasa yamebadilishwa kuwa hospitali za muda.
Wakati huo huo, China inachunguza njia za kukabiliana na mlipuko huo. Wanasayansi wake wanafanya kila wawezalo kuzindua chanjo mahsusi kwa ajili ya maradhi hayo. Nchini China, zaidi ya wahudumu wa afya 11,000 wametumwa mjini Wuhan, ikiwa ni pamoja na zaidi ya wataalamu 3,000 wa kushughulikia wagonjwa wenye hali tofauti. Hizi ni juhudi madhubuti kwa ajili ya kupigana na virusi vya Korona.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesifu jitihada za China katika kukabiliana na mlipuko huo.
"Ukweli kwamba hadi sasa tumeshuhudia maambukizi 68 tu nje ya China na hakuna vifo ni kwa sababu ya juhudi za ajabu ambazo China imeweka. Wanafanya hivyo bila kujali hali ya uchumi wao. "alisema Tedros.
Lakini licha ya juhudi hizi, baadhi ya nchi bado zinahoji taratibu zinazotumiwa na China kuzuia kuenea kwake. Mpaka sasa, baadhi ya mataifa yametoa taadhari kwa raia wao kutoingia China. Idadi kubwa ya mashirika ya ndege yamesimamisha safari zake kuelekea miji mbalimbali nchini China.
Wakati huo huo, ripoti nyingine za habari hazisaidii hali nchini China kwani zinaonekana kuwa na lengo la kuzua hofu kwa kutia chumvi kiwango cha mlipuko huo. Hadi sasa ripoti nyingi zimekuwa za kupotosha.
Itagharimu mshikamano wa kimataifa na msaada mahsusi kuweza kukabiliana na janga lenye kiwango cha mlipuko huu wa korona.
Kutokana na hali yao ya kiuchumi, mataifa ya Magharibi yanapaswa kutoa vifaa muhimu vya matibabu na chochote kinachohitajika katika vita hivi.
Ukweli ni kwamba, sisi ni kitu kimoja. 'Different colors, one people', Lucky Dube angesema. Uwe Mchina, Mwafrika, utoke Ulaya, au Marekani. Sisi sote ni sawa, na sasa zaidi ya hapo awali, tunahitaji kusimama kama kitu moja.
Kwa hiyo, inatia moyo kuona mashirika kama vile Bill na Melinda Foundation zikiahidi kutoa mchango wa dola 100,000,000 kusaidia juhudi za kupata chanjo ya kupunguza makali ya korona, na kusimamisha kuenea kwake pamoja na kuboresha ugunduzi wake na matibabu yafaayo kwa wagonjwa.
UNICEF inasema kuwa inasafirisha tani sita za barakoa ya kupumua na suti za kinga ili kuwalinda wahudumu wa afya nchini China.
"Virusi vya Korona vinaenea kwa kasi na ni muhimu kuweka rasilimali zote muhimu kwa ajili yake," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore.
Mlipuko huu wa virusi vya korona hatimaye utashindwa, lakini jumuiya ya kimataifa linapaswa kuhamasisha utoaji wa msaada kwa China unaohitajika katika hali hii isiyo ya kawaida.
Maelezo ya Picha:
Wahudumu wa afya waliovalia sare za kinga wanamtibu mgonjwa aliyeambukizwa virusi vya korona katika hospitali ya Zhongnan ya Chuo Kikuu cha Wuhan mwezi uliopita.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |