Mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona ulitokea mwezi Disemba mwaka 2019 nchini China, ulianza kupamba moto wakati wa sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa kichina. Hali hiyo ilifanya maambukizi hayo kuenea kwa kasi kote nchini. Kutokana na kukabiliwa na janga hili la dharura, wafanyakazi wa matibabu walianza mara moja kufanya kazi mstari wa mbele kupambana na virusi hivyo, wakiwa wanakabiliwa na changamoto nyingi.
Katika kipindi cha mwanzo cha mlipuko wa maambukizi ya virusi, hakukuwa na utafiti wa kutosha kuhusu uwezo wa maambukizi ya virusi vya Corona, wahudumu wa afya walikabiliana na hatari kubwa ya kuambukizwa, mbali na hayo kutokana na ukosefu wa mpango wa pamoja wa matibabu, hakukuwa na uwezo wa kutosha kuwatibu wagonjwa. Changamoto nyingine kubwa ilikuwa ni ukosefu wa vifaa vya kujikinga. Madaktari wengi walijikuta wakiwa na mufa mfupi sana wa kula, kulala au hata kwenda msalani, na wachache waliokuwa na muda wa kuvaa nguo ya kujikinga, kuvaa nguo hizo kwa muda mrefu kuliwaletea matatizo mengine kama vile matatizo ya kupumua. Kufanya kazi kwa muda mrefu kulifanya miili yao kuwa katika shinikizo kubwa.
Vilevile kulikuwa na changamoto za kihisia na kisaikolojia, Wafanyakazi wa matibabu walikuwa wanawasiliana moja kwa moja na wagonjwa, na kukabiliwa na hatari kubwa ya kuambukizwa hata kufariki. Hali ya wao kuwa katika hatari ya kuambukizwa, na kuona uchungu wa wagomjwa viliwaongezea shinikizo la kisaikolojia. Ikumbukwe pia katika kipindi chote cha kupambana na maambukizi ya virusi, wafanyakazi hao walitengwa na familia zao, hata baadhi ya jamaa zao walihisi kujuta kutokana na upweke. Hayo yote yaliongeza shinikizo la kisaikolojia.
Hata hivyo, wafanyakazi elfu 40 wa matibabu waliotoka sehemu mbalimbali kote nchini China, walimiminika kwenda mkoani Hubei na hasa katika mji wa Wuhan, ambao ni kiini cha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi, na kuonesha uwajibikaji mkubwa na moyo wa dhati wa kuwahudumia wagonjwa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |