Miaka 32 iliyopita Mao Yin kutoka mkoa wa Shanxi aliyekuwa na umri wa miaka miwili alitekwa nyara kwa udanganyifu kwenye mlango wa hoteli. Hivi karibuni polisi wa mikoa ya Shanxi na Sichuan walishirikiana kumsaidia kupata wazazi wake baada ya kufanya uchunguzi wa makini na kutumia data za DNA, na familia yake ilijumuika mjini Xi'an.
Hii ni moja kati ya kesi zilizoshughulikiwa kwenye operesheni maalumu ya idara za usalama wa umma kote nchini China dhidi ya uhalifu wa utekaji nyara wa watoto na wanawake. Hadi sasa idara za usalama wa umma kote nchini China zimefanikiwa kuwapata watoto zaidi ya 6,300 waliotekwa nyara miaka mingi iliyopita kwa kutumia data za DNA.
Takwimu kutoka mahakama kuu ya China zimeonesha kuwa, kuanzia mwaka 2013 hadi 2019, mahakama mbalimbali za China zimeshughulikia kesi zaidi ya elfu 28 za ukiukaji wa haki za watoto, zikiwa ni pamoja na kuwateka nyara, kuwafanyia dhuluma au kuwalazimisha kuombaomba barabarani, na wahalifu karibu na elfu 30 wamehukumiwa. Mahakama kuu pia inasisitiza kuwa, itatoa hukumu kali dhidi ya wahalifu waliokiuka vibaya sheria, na inapaswa kutoa hukumu ya kifo kwa wale wanaokiuka sheria vibaya zaidi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |