Mwanamke mmoja kutoka eneo la Majengo Nyeri alizua kisanga alipompigia kijana magoti akitaka amuoe baada ya kukosa mume licha ya kutamani kuwa na familia. Duru zinaarifu kwamba kisura huyo alikuwa amewakataa wanaume waliomtaka awali akisema hawakuwa wa hadhi yake, akiwemo kijana huyo. Inasemekana jamaa alikuwa mmoja wa wanaume waliomtongoza mrembo awali lakini alimkataa kwa dharau, na baadaye alifanikiwa kupata kazi ya jeshi na katika hali hiyo akafanya maendeleo ikiwemo kujenga nyumba nzuri na kufungua biashara.
Hata hivyo baada ya mwanamke kuzurura kwa miaka mitatu bila mafanikio alipata habari kuhusu mafanikio ya kijana huyo na ndipo akaanza kumsaka.
Hivi majuzi mmoja wa marafiki za jamaa alimuarifu kipusa kwamba alitarajiwa kuwepo nyumbani na hivyo iwapo angetaka kukutana naye aende kumtegea sokoni. Demu alijipura vilivyo siku hiyo na kuelekea alikoambiwa kumtegea mwanamme huyo akiwa na matumaini kuwa angekubaliwa. Hata hivyo walipokutana, jamaa alimpuuza kidosho na kujipa shughuli. Demu alipoona hivyo, alikimbia mbele ya jamaa akapiga magoti huku akimuomba amkubali.
Alipomweleza kijana nia yake ya kuolewa naye, kijana huyo alikataa na kusema amempata anayempenda kwa dhati, asiyeangalia utajiri au umasikini wake.
Dada alijitetea kwa kuomba asamehewe na kumtaka jamaa asahau yaliyopita. Akaendelea kujipendekeza kwamba yuko tayari kuanza maisha na yeye na kudai eti alikuwa amepofuka kwa kukosa hekima. Hata hivyo jamaa aliendelea kumtolea nje kwa kutoa dukuduku lake moyoni kwamba huko nyuma alimdharau sababu hakuwa na chochote. na kumhoji kwamba leo hii ameona ameendelea ndio anamhitaji?
Kwa mujibu wa habari demu alibaki sokoni akiwa amekauka kwa aibu na masikitiko kwa kumdharau jamaa hapo awali. Watu walimcheka huku wengine wakimtani kwa kujipendekeza kwa lofa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |