Hivi karibuni wizara ya usalama wa umma ya China imetoa ripoti kuhusu kazi ya kupambana na utapeli wa mtandaoni kwa mwaka huu. Takwimu zinaonesha kuwa tangu Januari mosi hadi leo, polisi nchini China wameshughulikia matukio elfu 16 ya utapeli kupitia mitandao ya Internet na ya simu, na kuwakamata washukiwa 7,506. Kwenye kipindi cha mlipuko wa virusi vya Corona, matukio ya utapeli kwa kisingizio cha kuuza barakoa na vifaa tiba mtandaoni yameripotiwa kwenye sehemu nyingi nchini China.
Mkurugenzi wa kitengo cha upelelezi wa uhalifu wa utapeli wa mtandaoni cha Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai iliyo chini ya Wizara ya usalama wa umma Bw. Lou Xiandi, amesema wizara hiyo inatilia maanani kesi za aina hiyo, na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kila kesi inatatuliwa kwa ufanisi.
Kwanza, upelelezi wa kila kesi unaitishwa na wizara moja kwa moja, na kutekelezwa na Kituo cha Taifa cha Kupambana na Utapeli. Baada ya kuthibitisha maficho ya matapeli, idara ya polisi ya huko inapewa taarifa ya kuwakamata. Huu ndio utaratibu wa kutatua matukio ya utapeli mtandaoni.
Pili, kuweka mkazo katika kuzuia uhalifu wa utapeli, kupitia kuongeza juhudi za upelelezi kabla ya matukio kama hayo kutokea. Wizara ya usalama wa umma itashirikiana na mashirika ya huduma za mitandaoni, ili kupeleleza na kuzuia matukio ya utapeli. Kama wakigundua maficho ya matapeli au genge fulani la matapeli wamepanga kufanya utapeli kupitia mitandao, watatoa taarifa mara moja kwa idara zote husika.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |