• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Hatua madhubuti za China za kukomesha matumizi mabaya ya data

    (GMT+08:00) 2020-09-11 10:25:20

    Na Eric Biegon – NAIROBI

    Juhudi za kimataifa za kuwalinda watumiaji wa teknolojia ya kidijitali pamoja na juhudi za kusitisha matumizi mabaya ya data, yalipigwa jeki wiki hii baada ya China kuzindua mwongozo inayokusudiwa kuhakikisha usalama wa habari na uendelezaji wa uchumi wa kidijitali ambao unaendelea kupanuka kila uchao.

    Katika kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu udhibiti wa sekta ya dijitali liliyofanyika Beijing, China linaonekana kuchukua uongozi kwenye kampeni za kuafikia usalama wa data kote ulimwenguni.

    Katika wito wake wakati wa mkutano huo, nchi hiyo yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani ilidumisha kwamba mataifa yana jukumu la kuhakikisha usalama wa data muhimu na habari za kibinafsi haswa ikizingatiwa kuwa kwa kawaida zina athari za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa nchi.

    Akihutubia mkutano huo uliowaleta pamoja maafisa wa serikali za kigeni na wenyeji, wasomi pamoja na kampuni kubwa kwenye sekta ya teknonojia ulimwenguni, Waziri wa Mambo ya nje wa China Wang Yi alibainisha kuwa nchi yake imekuwa ikifanya kila juhudi ili kufuata sheria kali za usalama wa data.

    Alisema kuwa utawala wa nchi yake chini ya chama cha kikomunisti cha CPC haujawahi na kamwe hautatoa shinikizo kwa kampuni za Wachina kuhamisha data kwa kukiuka sheria za nchi zingine.

    Na ni kutokana na hali hii ndipo waziri huyo alihimiza mataifa mengine kufuata nyayo za China.

    "Tunakaribisha serikali, mashirika ya kimataifa, kampuni za ICT, jamii za teknolojia, mashirika ya kiraia, watu binafsi na watendaji wengine wote kufanya juhudi za pamoja za kukuza usalama wa data chini ya kanuni ya mashauriano, mchango wa pamoja na faida za pamoja." Alisema

    Aliendelea kushutumu majaribio ya baadhi ya nchi ambazo alizituhumu kwa kutafuta kupata habari kwa njia zisizo halali.

    "Hatujauliza na hatutauliza kampuni za Wachina kuhamisha data nje ya nchi kwa serikali kwa kukiuka sheria za nchi zingine." Wang alikariri

    Wakati ambapo changamoto zinaendelea kujitokeza katika sekta hii, China inaamini kwamba mpango wa ulimwenguni wa usalama wa data uliozinduliwa siku ya jumanne, utahakikisha kukomeshwa kwa matumizi ya teknolojia ili kudhoofisha miundombinu muhimu katika mataifa mengine au kuendeleza ulaghai wa upatikanaji wa data muhimu.

    "Lazima tuchukue hatua kuzuia na kukomesha shughuli zinazokiuka habari za kibinafsi, kupinga matumizi mabaya ya ICT kufanya ufuatiliaji wa watu wengi dhidi ya Mataifa mengine au kushiriki katika ukusanyaji wa habari za kibinafsi zingine bila idhini." Waziri huyo alisema.

    Lakini mbali na serikali, China inataka kampuni zinazofanya kazi katika mataifa ya nje kuheshimu sheria za nchi zinazohudumu, na kuacha kulazimisha kampuni za ndani kuhifadhi data zilizozalishwa na kupatikana nje ya nchi hizo.

    Serikali ya Rais Xi Jinping inasisitiza kwamba mataifa lazima yaheshimu uhuru, mamlaka na utawala wa data ya mataifa mengine, na lazima wakati wote yakatae hamu ya kushinikiza kampuni au watu binafsi kutoa data iliyoko katika nchi nyingine bila idhini.

    Lakini ikiwa data inayohusika ina umuhimu mkubwa sana kwa taifa au serikali, basi China inapendekeza kwamba hii inapaswa kuwezeswa kupitia usaidizi wa kimahakama au njia zingine zinazofaa kisheria.

    Wang hata hivyo alionya watoa huduma za ICT dhidi ya "kutumia milango ya nyuma" katika huduma zao ili kupata data ya mtumiaji kinyume cha sheria.

    "Kampuni za teknolojia hazipaswi kutafuta maslahi haramu kwa kutegemea watumiaji wa bidhaa zao." Alisema

    Huku likihimiza mataifa yote kuunga mkono mpango huu, China inasisitiza kwamba nchi zinapaswa kuzingatia fursa zinazotokana na maendeleo ya dijitali ili kuimarisha ushirikiano ambao utasababisha maendeleo.

    Shinikizo hili la hivi karibuni kutoka China linafanyika baada ya hatua za hivi karibuni za Marekani kuzindua mpango uliopewa jina "Mtandao safi" ambao unaonekana kuwa jaribio la kuzipiga vita baadhi ya kampuni za kigeni zinazohudumu ndani ya mipaka yake.

    Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya uzinduzi huu, utawala wa Rais Donald Trump uliweka vikwazo kwa kampuni za Marekani zinazofanya biashara na kampuni ya Huawei, ambayo ndio kubwa zaidi ya teknolojia nchini China. Aidha kuna mpango wa kupiga marufuku apu za TikTok na Wechat huko Marekani kwa kile serikali ya Trump kinataja kama tishio la usalama wa taifa hata ingawa bado haijatoa ushahidi kuhusiana na madai hayo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako