• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ustadi mkubwa wa opera ya Sichuan

    (GMT+08:00) 2008-12-02 16:18:33

    Mchezo wa opera ya Sichuan ulitokea zaidi ya miaka 100 iliyopita, mchezo huo umekuwa ukipendeza sana kutokana na uimbaji wake wa kuvutia, miondoko ya kupendeza na maneno ya kufurahisha ya wachezaji. Mchezaji mashuhuri wa opera ya Sichuan, Bw. Lan Jiafu alishiriki shughuli za mchezo huo kwa zaidi ya miaka 30. Alisema, opera za sehemu nyingine ikiwemo opera ya Kun ziliingia katika mkoa wa Sichuan na kuchanganyana na opera ya taa ya huko, zikaendelezwa kuwa opera ya Sichuan. Kwa kulinganishwa na opera za sehemu nyingine, opera ya Sichuan ina umaalumu pekee wa jadi ya utamaduni na sanaa. Alisema:

    "Kuna opera kadhaa kubwa nchini China, ambazo ni pamoja na opera za Sichuan, Beijing na Henan. Umaalumu wa opera ya Sichuan unaendana na umaalumu wa utamaduni wa huko, wachezaji wanasema maneno mengi ya kufurahisha watu, maonesho ya mchezo yanaambatana sana na hali halisi ya maisha ya watu, hivyo inaeleweka kabisa, hususan uimbaji wa opera ni wa kipekee, na unaendana na desturi za maisha ya wenyeji wa Sichuan. Zaidi ya hayo, kuna mambo mengi madogo madogo katika maonesho ya mchezo, kama vile, mchezaji anabadilisha mara kwa mara kinyago anachovaa usoni, kuficha upanga, kujitwika bakuli na kucheza mishumaa."

    Ustadi mkubwa wa opera ya Sichuan ni mchezaji kubadilisha mara kwa mara kinyago anachovaa usoni. Karibu kila mtu anaposikia watu wakitaja opera ya Sichuan, anafikiri mara moja "kubadilisha kinyago cha usoni", sasa karibu imekuwa alama ya kipekee ya opera ya Sichuan. Katika sauti ya muziki wa opera, mchezaji anajisitiri kwa mkono wa nguo yake, baada ya kutingisha kichwa chake, mara moja anajitokeza akiwa amevaa kinyago kingine usoni mwake, ustadi mkubwa huo unawashangaza kabisa watazamaji.

    Kila mtazamaji aliyeangalia maonesho hayo, anataka kujua siri yake, lakini kila mchezaji wa opera ya Sichuan huwa ananyamaza kimnya, na hataki kabisa kufichua siri hiyo. Mchezaji kijana, Bw. Chen Jiaxin alisema, ustadi wa kubadilisha kinyago ni wa siri kubwa ya watu wanaohusika na opera ya Sichuan.

    "Kubadilisha kinyago cha usoni ni ustadi mkubwa wa mchezaji, kuna mbinu za aina tatu, na zote ni siri kabisa. Mchezaji anaweza kufika hadi kubadilisha mara tatu kinyago cha usoni katika sekonde moja tu."

    Ili kufahamu siri ya mbinu ya kubadilisha kinyago cha usoni, tulimtembelea profesa wa chuo kikuu cha Sichuan, ambaye ni msomi kuhusu mila na jadi za watu, Bw. Mao Jianhua. Alisema, kuna mbinu za aina tatu zinazotumiwa katika kubadilisha kinyago cha usoni, yaani kupaka, kupuliza na kukwanyua. Kupaka ni kupaka mafuta ya rangi kwa mkono, wakati mafuta ya rangi yanaposogelea karibu na uso, uso ukawa na rangi ya aina nyingine. Mbinu ya kupuliza ni kupuliza unga wa rangi ya dhahabu, nyeusi na rangi ya fedha. Wakati wa maonesho, iliwekwa mkebe mmoja kabla kwenye jukwaa la maonesho, ndani ya mkebe huo kuna unga wa rangi, wakati mchezaji anapojiviringisha chini, anasogeza uso wake kwenye ule mkebe na kupuliza unga uliomo ndani ya mkebe, uso wake ukawa na rangi ya aina nyingine. Mbinu ile inayotumiwa mara nyingi zaidi ni ile ya kukwanyua.

    "Kwa kawaida mbinu tunayoiona, ambayo inatumiwa na mchezaji ni kukwanyua kinyago cha usoni. Vinyago vinachorwa kwenye kitambaa cha hariri na kubandikwa usoni kimoja baada ya kingine, vinyago hivyo vinafungwa kwa nyuzi nyembamba, ambazo zinafungwa sehemu zinazoweza kufikiwa na mkono katika nguo yake, lakini watazamaji si rahisi kuziona. Wakati maonesho ya opera yanaendelea, mchezaji huwa anacheza huku akikwanyua kinyago kimoja kimoja. Kufanya hivyo si kazi rahisi. Endapo vinyago vilibandikwa imara sana usoni, mchezaji atashindwa kuviondoa, pengine anaweza kuviondoa vinyago vyote kwa pamoja, tena mchezaji anapaswa kutenda vitendo vingine vya kuficha, kusudio lake la kukwanyua kinyago ni kuwafanya watazamaji wasiweze kuona kitendo chake cha kukwanyua kinyago cha usoni."

    Hata hivyo, watu watauliza, katika maonesho, mchezaji hukwanyua vinyago zaidi ya kumi, je, vinyago vilivyoondolewa usoni, viliwekwa wapi? Vinyago vile vya ajabu vilitengenezwa namna gani? Siri yake iko wapi? Mambo hayo ya kiufundi, pengine watu wa kawaida kama sisi, kabisa hatuwezi kuyafahamu, isipokuwa tunafikiria tupendavyo. Kama mchezaji wa opera ya Sichuan, Bw. Lan Jiafu alivyosema kuwa hivi ndivyo vitu vya kuvutia vya opera ya Sichuan.

    "Kubadilisha vinyago ni kazi ya ustadi, mtu akifanya shughuli za sekta hiyo, anazuia siri hiyo, kama mchezaji wa mchezo wa kiini macho anavyofanya, akitoboa siri ya mchezo, basi mchezo wake hautashangaza watu tena."

    Ustadi mwingine unaolingana na ustadi wa kubadilisha kinyago cha usoni katika opera ya Sichuan ni kutoa moto mdomoni. Mchezaji anajiweka tayari kwanza, kisha anatoa moto mkubwa mdomoni, ni hali ya kushangaza na kufurahisha sana. Inasemekana kuwa mchezaji anatoa moto mdomoni, kwanza anaweka mafuta ya taa mdomoni mwake, halafu anapuliza kwa nje mafuta ya mdomoni, mafuta yakawa kama ukungu na kuwaka moto; mwiko kwa mchezaji kuvuta pumzi wakati moto haujazima, la sivyo, matokeo yake ni kujiwasha moto. Mchezaji wa kutoa moto mdomoni wa opera ya Sichuan, Bw. Li Ke alisema, kutoa moto mdomoni mara kwa mara inafanyika pamoja na kubadilisha kinyago cha usoni ili kuongeza uzuri wa mchezo na hali ya kuvutia.

    "Kutoa moto mdomoni ni umaalumu mkubwa mwingine wa Opera ya Sichuan, hii inaambatana na kubadilisha kinyago cha usoni. Maonesho hayo mawili yanashirikiana na kutiliana nguvu. Hebu tutoe mfano, wakati wa kufanya maonesho ya mavazi ya fashion pasiwepo na taa, maonesho yanapendeza? Bila shaka hayapendezi watu. Ni tofauti kabisa, maonesho yanafanyika huku wachezaji wanaangazwa kwa taa kubwa na maonesho yanayofanywa bila mwangaza mkubwa. Vivyo hivyo, kutoa moto mdomoni kunaongeza mvuto wa maonesho ya kubadilisha kinyago cha usoni."

    Katika opera ya Sichuan, kuna ustadi mwingine wa kutoa ghafla maua na kuficha mara moja upanga. Kidogo mambo hayo ni kama mchezo wa kiini macho, mchezaji akiwa na mikono miwili mitupu, lakini anaweza kutoa maua ghafla mara kwa mara; kuficha upanga kunategemea ustadi wa mchezaji kutenda vitendo kwa haraka mno, mchezaji akiwa mbele ya watazamaji wengi, ghafla upanga uliokuwa mkononi mwake unatoweka kabisa, upanga haukupotea isipokuwa ulifichwa kwa haraka na mchezaji mwilini mwake.

    Katika mji wa Chengdu, mkoa wa Sichuan, kila siku watu wanaweza kuona maonesho ya opera ya jadi ya Sichuan, ambapo wanakunywa chai au kula chakula kingine, huku wakiburudishwa na opera ya Sichuan, huu ni mtindo wa kawaida wa wenyeji wa Sichuan. Majumba yanayofanya maonesho ya opera ya Sichuan katika mji wa Chengdu ni pamoja na ya Wuhouci, Shunxing na Kituo cha maonesho ya sanaa ya opera ya Sichuan. Mkurugenzi wa mgahawa wa chai wa Shufengyayun, ambapo yanaoneshwa maonesho ya opera ya Sichuan, Bw. Li Xian alisema, opera ya Sichuan inaoneshwa kila siku bila kujali kunyesha mvua au kuvuma upepo mkubwa. Alisema:

    "Opera inaoneshwa kila siku saa 2 usiku katika miaka 10 iliyopita, tunafanya maonesho kila siku hata kama yuko mtazamaji mmoja tu. Tunashikilia kufanya hivyo kuhusu opera ya Sichuan, vilevile kama ni imani yetu, bila kujali maonesho yanapata faida au la. Katika baadhi ya nyakati ambazo kuna watazamaji wengi, tunafanya maonesho mawili kila siku, kila onesho lina watazamaji 800, maonesho yetu yanapendwa na watu wa nchini, hata katika nchi za nje."

    Opera ya Sichuan inavutia watazamaji wa sehemu mbalimbali za dunia, wana shauku kubwa ya kuona ustadi wa ajabu wa mchezaji wa kubadilisha kinyago anachovalia usoni katika maonesho ya opera ya Sichuan, na wanashangilia. Mtalii kutoka Yemen, Bw. Asaada M. Shugaa Addin baada ya kuona maonesho ya opera ya Sichuan, alisema,

    "Hi ni mara yangu ya kwanza kufika Chengdu, opera ya Sichuan inanivutia sana, huu ni mchezo wa jadi kabisa wa China, ambao unawakilisha utamaduni wa China. Ninapenda sana kiini macho cha kubadilisha kinyago cha usoni, inanishangaza kwelikweli."


    1 2
    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako