Operesheni ya jeshi la Israel ya kuushambulia ukanda wa Gaza kwa ndege iitwayo Cast Lead tarehe 29 iliingia siku ya tatu.
Kwa mujibu wa ripoti ya jeshi la Israel, jeshi hilo liliushambulia ukanda wa Gaza kuanzia usiku wa tarehe 28 hadi asubuhi ya tarehe 29. Viwanda vya silaha, maghala ya makombora, vituo vya kuangalia, vituo vya kurusha makombora, maghala na mahandaki 50 yaliyoko kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri ya kundi la Hamas yaliteketezwa. Jeshi la maji la Israel lilifaulu kushambulia meli na vituo vya kuangalia vya kundi la Hamas kwa mizinga. Kuanzia tarehe 27 ukanda wa Gaza ulishambuliwa na jeshi la Israel kwa ndege kwa mara zaidi ya 300, hadi hivi sasa watu zaidi ya 320 wameuawa, na wengine 1400 wamejeruhiwa.
Tarehe 29 asubuhi kundi la watu wenye silaha la Palestina lilirusha makombora mengi dhidi ya Israel, na waliua na kujeruhi watu zaidi ya 20. Tarehe 29 mchana, , mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya ukanda wa Gaza kwa ndege yalipungua kidogo kutokana na sababu ya hali ya hewa, lakini matayarisho ya jeshi la nchi kavu yanaendelea haraka. Hadi saa 12 jioni, matayarisho ya jeshi la nchi kavu yalimalizika. Habari zinasema matayarisho hayo yalifanyika kwa ajili ya kipindi cha pili cha operesheni ya kijeshi ya "Cast Lead".
Operesheni ya jeshi la Israel huko Gaza itakuwa na athari kubwa kwenye hali ya Mashariki ya Kati ikiwemo Israel.
Kwanza, viongozi wa serikali ya Israel wana maoni tofauti kuhusu operesheni hiyo. Waziri wa sayansi, utamaduni na michezo wa Israel Bw. Raleb Majadele ambaye ni mwarabu hakuhudhuria mkutano wa baraza la mawaziri kuhusu opereheni ya kijeshi dhidi ya Gaza ili kuipinga operesheni hiyo, na alitoa mwito wa kuitaka serikali isifanye hali ya huko kuwa ya wasiwasi zaidi, na kulitaka kundi la Hamas lisimamishe mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel. Tarehe 29 kwenye mkutano maalumu wa bunge kuhusu operehesni hiyo, mbunge wa kiarabu Bw. Ahmad Tibi alilaani wazi kuwa viongozi wa serikali walifanya uamuzi huo kutokana na maslahi binafsi, na walitaka kujipatia viti vya bunge kwa mwili wa Wapalestina.
Pili, operesheni hiyo ya kijeshi iliongeza matatizo kwa Jordan na Misri ambazo zinahimiza mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.
Operesheni ya jeshi la Israel huko Gaza huenda ikasababisha suala la wakimbizi. Ingawa hivi sasa suala hilo bado si wazi, lakini limetokea. Tarehe 28 matukio matano ya kuvuka mpaka yalitokea kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri wenye urefu wa kilomita 14. Watu walioshuhudia matukio hayo walisema watu walivunja ukuta mpakani kwa tingatinga, na Wapalestina mia kadhaa walikimbilia Misri.
Tatu, muda wa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas utamalizika tarehe 9 mwezi Januari mwakani. Mashambulizi dhidi ya ukanda wa Gaza kwa ndege ni jambo baya kwake. Mjumbe wa kwanza wa Palestina kwenye mazungumzo Bw. Ahmed Qureia tarehe 29 alisema mamlaka ya utawala wa Palestina ulisimamisha mazungumzo ya amani kati yake na Israel kwa muda, ili kupinga mashambulizi ya jeshi la Israel. Pia alisema Israel ikiendelea kufanya operesheni za kijeshi dhidi ya ukanda wa Gaza na kuwashambulia Wapalestina, mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili hayataanzishwa tena.
Nne, mazungumzo ya amani kati ya Israel na Syria yaliyoanzishwa tena mwezi Mei mwaka huu hayakugusia masuala halisi. Wakati hali ya Gaza inapokuwa ya wasiwasi zaidi, Syria ilisema mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yamezuia juhudi zote za kuhimiza mchakato wa amani wa kisiasa. Uturuki inayopatanisha suala hilo haina uwezo wa kutatua tatizo hilo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |