Ofisa mhusika wa China tarehe 6 hapa Beijing amesema, China itaendelea kuchukua hatua za kuhimiza soko la nyumba liendelezwe vizuri, na kulifanya soko hilo lioneshe umuhimu wake wa kupanua mahitaji ya nchini na kuhimiza ongezeko la uchumi; aidha China itaongeza nguvu ya kujenga nyumba kwa ajili ya kuboresha hali ya makazi ya watu wenye mapato ya chini.
Tokea nusu ya pili ya mwaka uliopita, kutokana na athari ya msukosuko wa fedha duniani na kupungua kwa ongezeko la uchumi nchini, pamoja na marekebisho ya soko lenyewe la nyumba na hali nyingine mbalimbali, hali ya kuzorota imeonekana katika mauzo ya nyumba nchini China. Hivyo serikali ya China imetoa sera mfululizo za kuhimiza maendeleo ya soko la nyumba.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 6, naibu Mkurugenzi wa ofisi ya mambo ya utawala ya kodi katika wizara ya fedha ya China Bibi Wang Xiaohua alisema:
Marekebisho ya sera huenda yataonesha ufanisi wake baada ya muda fulani, mwaka 2008 serikali ya China imetoa sera za marekebisho mbalimbali juu ya kodi kwenye soko la nyumba, kama sera hizo zitatekelezwa vizuri huenda zitaendelea kutekelezwa, na kama hazitatekelezwa vizuri, huenda serikali itazingatia kuchukua sera na hatua nyingine nzuri zaidi.
Wakati wa kuhimiza soko la nyumba liendelezwe vizuri, serikali ya China pia inatilia maanani kuwasaidia watu wenye mapato ya chini wapate nyumba mpya. Kwa kufuata mpango, China inatazamiwa kutumia miaka mitatu kutatua suala la makazi ya watu wa familia zenye mapato ya chini zipatazo milioni 75, na kuwasaidia wakazi wa familia zipatazo milioni 24 ambao bado wanaishi kwenye nyumba za hali duni wahamishwe au kuwasaidia kukarabati nyumba.
Naibu waziri wa nyumba na ujenzi wa miji na vijiji wa China Bw. Qi Ji anaona kuwa, kuongeza ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watu wenye mapato ya chini hakutaweza kuathiri soko la nyumba za biashara. Alisema:
Kufanya hivyo kutasaidia kutatua taabu halisi za wananchi, pia kutabainisha zaidi soko la nyumba. Watu wenye mapato ya chini watatatua suala lao la makazi kwa msaada wa serikali, na watu wengine wanaweza kununua nyumba au kukodisha nyumba kwa kupitia soko.
Imefahamika kuwa, serikali kuu ya China imeongeza fedha za kusaidia ujenzi wa nyumba zenye bei chini na kukarabati nyumba za hali duni. Katika mpango uliotolewa na serikali ya China kuhusu kutenga fedha trilioni 4 kwa ajili ya kupanua mahitaji ya nchini, mtaji mkubwa utawekwa katika ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watu wenye mapato ya chini. Aidha, idara husika za serikali ya China zimetoa sera za kutoa kipaumbele kwa kupanga ardhi ya ujenzi wa nyumba hizo. Naibu waziri wa nyumba na ujenzi wa miji na vijiji Bw. Qi Ji alisema:
Kama iko siku uchumi wa China utaendelezwa vizuri zaidi, na mapato ya wananchi yataongezeka zaidi, serikali ya China bado itabeba wajibu wa kuwasaidia watu wa familia zenye mapato ya chini kushinda taabu za makazi, yaani bado ingewajibika kujenga nyumba kwa ajili ya watu hao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |