• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji 0317

    (GMT+08:00) 2009-03-17 19:03:29

    Wiki mbili zilizopita, tulipata barua kutoka kwa msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff ambaye alisema jambo lingine ambalo sitaweza kusahau ni kuwa kipindi cha sanduku la barua kilibadilishwa na kuwekwa jumanne saa 4.00 usiku na mara nyingine Jumamosi saa 4.00 usiku. Hata hivyo kulingana na tangazo ambalo liko kabla ya kusoma makala kutoka China bado tunafahamishwa kuwa matangazo yanatufikia kutoka saa 9.00 -10.00 alasiri. Kuanzia jumatatu hadi jumamosi na kuanzia saa nane mchana mpaka saa tisa mchana. Lakini kulingana na mambo yalivyo makala haya kwa muda sasa yanasikika saa nne usiku toka jumatatu mpaka jumamosi. Na saa kumi na moja jioni jumapili. Hii ina maana kuwa kulingana na shirika la habari la Kenya-KBC kuna mabadiliko makubwa sasa ikiwa tangazo lile litabaki vivyo hivyo litapotosha wasikilizaji wengi haswa wageni.

    Kuhusu jambo hilo, mwanzoni tumelirekebisha tangazo letu kabla ya matangazo yetu kwa kupitia KBC, kwani ni ombi lililotolewa na wengi na inaonekana kuwakera watu, kwa kuwa hatupendi kuwaudhi wasikilizaji wetu, lakini tulidhani matangazo hayo yanatangazwa kila siku saa 11 hadi 12 jioni, na jumamosi ni saa 9 hadi 10 alasiri, kwani tuliambiwa na KBC kwamba walitaka kurekebisha muda, lakini hatukukubali, tulidhani ingetangaza saa hiyo hiyo 11 hadi 12 jioni, kwa hivyo mpaka sasa tangazo tulilosahihisha bado lina makosa, hata mpaka wiki iliyopita tulithibitisha na kufahamu kwamba, kumbe KBC ilirekebisha saa ya matangazo yetu bila kutuarifu, hakika hili pia ni kosa letu, kwa kushindwa kugundua hali hii. Juu ya jambo hili tunalifuatilia,

    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161, Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anachukua fursa hii kuwapongeza sana waandishi ,wahariri na watangazaji wa idhaa ya Kiswahili ya CRI kwa kutayarisha vipindi maalumu vya sherehe ya mwaka mpya wa kilimo wa jadi wa nchini China, shamrashamra zilizoanza tarehe 26 hadi tarehe 30 mwezi januari 2009.Baadhi ya watangazaji hodari wa idhaa ya Kiswahili ya CRI mama Chen,Han Mei,Pomboo,Pili Mwinyi ambaye ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili kutoka Tanzania(Zanzibar) wakishirikiana na wageni waalikwa wanafunzi kutoka Tanzania wanaosoma nchini China ndugu Emanuel Moses Onasaa na ndugu Ramadhani Mtoro pia na bwana P.K kutoka jamhuri ya Kenya,wote kwa pamoja mlitupatia burudani nzuri sana kuhusu mwaka mpya wa jadi wa kilimo wa china.

    Pia balozi wa Tanzania nchini China mheshimiwa Omari Mapuri alisema maneno machache na kututakia heri ya mwaka mpya wa jadi wa kichina na tunamshukuru.

    Kwa hakika washiriki wote kwenye matangazo hayo maalum ya shamrashamra za mwaka mpya wa jadi wa kichina walifanya kazi nzuri na walimudu kuelezea vizuri kuhusu walivyowaona wachina wakiadhimisha sherehe hizo murua. Pamoja na hayo mlitujulisha kuhusu upigaji fataki na fashifashi ikiambatana na kuweka mapambo milangoniļ¼Œkupeana zawadi(pesa) baina ya watoto na wazazi(wakubwa).Pia uandaaji na upikaji wa chakula maalumu kwa ajili ya mwaka mpya, na kucheza michezo mbalimbali ya kiutamaduni . Aidha wanyama12 ambao huwa alama ya kila mwaka mnyama mmoja kwa kalenda ya kichina ambapo inapotimia miaka 12 ni duru moja na hivyo kuanza tena kwa kurudia wanyama hao hadi miaka mingine 12.

    Mlitujulisha pia kwamba mwaka huu wa 2009 ni mwaka wa ng'ombe.Mimi nimefurahi kweli kwa kuwa mimi ni mmojawapo wa watanzania wanaofuga ng'ombe .Napendelelea zaidi nyama ya ng'ombe na kuku.Wanyama hao 12 wa kuwakilisha utamaduni na jadi ya wachina ni ustadi na ubunifu mkubwa na wa thamani kubwa uliofanywa na ndugu zetu wachina na unapaswa kuendelezwa vizazi na vizazi,ama karne na karne.

    China ina utajiri sio wa maliasili tu,lakini hata utamaduni wake ni wa kiwango cha juu sana,na sidhani kama China inaweza kuathiriwa na utandawazi kama zilivyoathiriwa nchi nyingi duniani.Wananchi wa China wapo makini sana kwa kila kitu na ninawapongeza sana kulinda na kudumisha mila na desturi zao ambazo si kivutio kwao tu, lakini hata kwa wageni na watalii wote wanaopata fursa ya kutembelea China na kuziona.

    China ina makabila 56 tofauti,serikali kuu na mamlaka nyingine za kitaifa na kimkoa zinalinda na kuhifadhi utamaduni ,mila na desturi za makabila yote,yakiwemo makabila madogomadogo ya china.Huu ni mpango mzuri sana kwa kuwa unalinda heshima na asili ya binadamu katika nchi husika.

    Taifa la China litafanikiwa katika mambo mengi mazuri kwa kiwango cha juu sana.Hongereni sana.

    Shukrani sana msikilizaji wetu Kilulu Kulwa kwa kweli tumefurahi sana kuona kwamba wewe ni mmoja kati ya wasikilizaji wetu waliotutegea vizuri sikio na kufuatilia vipindi vyetu vya mwaka mpya wa jadi wa China kwa karibu na kujua kwamba wewe na wengine mumeweza kufahamu utamaduni wa China na mambo mbalimbali yanayohusiana na sherehe .

    Hivi karibuni tumepata barua pepe nyingi kutoka kwa wasomaji wetu kwenye tovuti ya mtandao wa internet.

    Waringa estwarm@yahoo.com amesema katika barua yake pepe kuwa, tovuti ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa hunifurahisha sana kwa utangazaji wake wa kuvutia na pia makala zake mbalimbali pia zilinifurahisha sana!

    Msomaji wetu kwenye tovuti ya Kiswahili ya mtandao wa internet Bw. Epafara Stanley wa epst01@hotmail.com ameacha maoni yake akisema, matangazo yenu kwa njia ya tovuti ninayapata vizuri kabisa.

    Msomaji wetu kwenye tovuti ya Kiswahili ya mtandao wa internet Bw. Telly-Wambwa wa sanduku la posta 2287, Bungoma Kenya amesema kwenye barua yake pepe kuwa, mikutano miwili ya mwaka ya Bunge la umma la China na Baraza la mashauriano ya kisiasa la China iliyofanyika hivi karibuni mjini Beijing ilikuwa na umuhimu mkubwa hasa imelingana na matarajio ya bara la Afrika. Sisi tunaweza kujifunza mengi kutoka kwa sera zinazofuatwa nchini China.

    Msikilizaji wetu Franz Manko Ngogo wa Kemogemba sanduku la posta 71 Tarime Tanzania ametutumia barua pepe akisema, ninazo shukran nyingi za dhati kwa watayarishaji wa kutufanya tupate habari mahsusi ya mikutano miwili ya Bunge la umma la China na Baraza la mashauriano ya kisiasa la China. Licha ya kuwa matangazo yenu sasa yanazidi kushika kasi lakini mbona vipindi vinazidi kufifia na badala yake tunasubiri mpaka siku ya sanduku la barua ndipo tunafurahi kiasi. Mwisho naomba picha zangu nilizopiga huko China nitumiwe. Ninazikumbuka sana.Samahani.

    Tunamshukuru Bw. Ngogo kwa barua yake na maoni yake juu ya vipindi vyetu hasa alivyosema kuwa matangazo yetu sasa yanazidi kushika kasi lakini mbona vipindi vinazidi kufifia, tutajitahidi kujirekebisha ili kuwafurahisha wasikilizaji. Lakini kwa kweli siku nyingi hatukuweza kupata barua nyingi zilizoeleza mambo halisi ambayo tunaweza kuyasoma, nyingi tulizopata ni kuhusu chemsha bongo, ni maneno machache na majibu tu. Kweli siyo kila mara tunaweza kupata barua iliyoandikwa mengi kama alivyotuletea Bw. Kilulu Kulwa, au Msabaha Mbarouk Msabaha. Hapa tunawataka wasikilizaji wetu waweze kutuletea barua za kutoa maoni na mapendekezo hata kueleza mambo mbalimbali mnayokuta katika kazi na maisha yenu, ili kuchangia kipindi chetu cha sanduku la barua.

    Msomaji wetu kwenye mtandao wa internet wa omanyengo@yahoo.com

    ametutumia barua pepe akisema, mimi Pastor Osborne Manyengo wa Rosa White Stone Life Centre wa sanduku la posta 260 Kitale-Kenya natoa salamu nyingi kwa watangazaji wa cri,nawapongeza kwa kazi yenu nzuri.

    Nashukuru kwa zawadi mliyonitumia nilipokea kwa moyo mkujufu kalenda ya mwaka huu na kadi za salamu na zawadi, hongera radio china kimataifa.

    Jambo ninaloweza kusema ni kwamba usomaji wa salamu ndio uko chini kidogo maana mtangazaji Bw. Moses anasoma kadi chache sana heri asome kama alivyosoma mtangazaji Bw Ramadhani maana kuna kadi nyingi sana huko na bado tunatuma zingine kwa wingi na kadi ziwe zinarudiwa mara mbili sio zaidi ya hapo.

    Nikimalizia naomba munitumie kitabu cha kujifunza kichina mimi nataka kujua kichina maana hivi karibuni natarajia kuja kutembea huko kwa mwaliko wenu. salamu zangu kwa mashabiki wote wa radio china kimataifa pamoja na wafanyakazi wa radio china hongera kwa vipindi vyenu murua nitaendelea kuchangia mijadala yenu na maoni mukinipa nafasi. pia naomba munitumie ile radio ya majira kutoka hapo.

    Msomaji wetu kwenye mtandao wa internet Norman Mjomba Majala ambaye barua zake huhifadhiwa na Boswell Mjomba P.O.Box 99779 Mombasa Kenya amesema, kwanza pokeeni salamu zangu za dhati toka kwangu. Uzima nilionao si wa kukadiriwa na kigongo, vilevile natazamia mu wazima. Pili nashukuru kutunukiwa cheti ya nafasi ya Tatu ikiandamana na foronya za kuvishia mito, katika chemsha bongo ya michezo ya Olimpiki ya China. Kusema kweli nimekawia sana kuwaandikia laiti ningepata nafasi ya kuitembelea China mamangu angelibubujikwa na machozi ya furaha, kwani alikuwa mwenye furaha isiyo na kifani siku hiyo, na hunipa motisha kubwa sana .Kwani nilimaliza kidato cha nne mwaka elfu mbili na sita na sio ajabu barua zenye chemsha bongo hazinifikii kiurahisi.

    Kwa sasa najifunza ufundi wa magari, nakama ingewezekana, mungefungua Ofisi ya Redio China Kimataifa hapa Mombasa , ili tupate chemsha bongo toka kwenye mtandao wenu kwa urahisi. Kwani kupata matangazo ya chemsha bongo kupitia mtandao katika tarakilishi za kibiashara hapa ni ghali.

    Fauka ya hayo, ningelikuwa naifahamu lugha ya China barabara, bila ya shaka,ningekua na marafiki wengi wa china hapa Mombasa .La kufurahisha ni kuwa hivi majuzi mamangu amepata naafasi ya kazi ya nyumbani kwa mchina. Nawatakia kila la kheri na rabana atujazie pumzi mara kwa mara tupate kufahamiana kila mara

    Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu kwa barua pepe mlizotutumia kuhusu suala la kadi tunamuambia Bw. Pastor Osborne Manyengo wa Kitale Kenya, kwamba muda wa kusoma kadi umepunguzwa na kipindi hiki cha salamu zenu lazima kiambatane na muziki, hata hivyo tutajitahidi kuongeza kadi zinazosomwa ili kuhakikisha kadi zote zinasomwa.

    Kutoka 'madaktari pekupeku' hadi hospitali za vijijini

    Kutokana na utekelezaji wa utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano vijijini, shughuli za huduma za matibabu vijijini nchini China pia zimeendelea kupiga hatua mbele, hospitali za vijijini zimepata maendeleo makubwa na hali ngumu kwa wakulima ya kupata matibabu imeboreka kidhahiri, kiwango cha huduma za matibabu kwa wakulima pia kimeendelea kuinuka.

    Wasikilizaji wapendwa, mliwahi kusikia "madaktari pekupeku"? 'madaktari pekupeku' ni matokeo maalumu ya historia ya huduma za afya za China, yaani madaktari wasioajiriwa rasmi na serikali na hawajapata elimu rasmi ya udaktari ambao walifanya matibabu vijijini katika miaka ya 60 hadi 80 ya karne iliyopita. Madaktari hao walitoka pande mbili, kwa upande mmoja walitokea katika familia za madaktari, kwa upande mwingine baadhi ya wahitimu wa shule ya sekondari au sekondari ya juu wanaofahamu kidogo ujuzi wa udaktari walichaguliwa na kupewa mafunzo ya muda mfupi, wakawa 'madaktari pekupeku'. Kwa kuwa hawakuwa na mshahara, baadhi yao pia walikwenda pekupeku mashambani na kufanya kazi za kilimo, ndiyo maana wakaitwa 'madaktari pekupeku'.

    Mjumbe wa Baraza la 11 la mashauriano ya siasa la China ambaye ni mwelekezaji wa daktari katika hospitali ya kwanza ya chuo kikuu cha udaktari cha Xinjiang Bi. Adalaiti Ahemaitijiang alisema:

    "kabla ya China itekeleze sera ya mageuzi na kufungua mlango kwa nje, kulikuwa na kundi la madaktari pekupeku, wote ni watoto wa vijijini, walipewa mafunzo ya miezi kadhaa, baadaye wakatibu wagonjwa kwa kutumia sindano akyupancha na mitishamba."

    Kwa kutumia vifaa hafifu vya matibabu pamoja na hamu kubwa ya kuhudumia watu wenye matatizo ya kiafya, madaktari hao walitoa huduma za kimsingi za afya kwa mamilioni ya wakulima, na walitoa mchango mkubwa kwa kutatua matatizo ya ukosefu wa dawa na ugumu wa kupata matibabu katika sehemu za vijijini wakati huo.

    Lakini magonjwa hayatibiki kwa hamasa tu, kutokana na kiwango cha chini cha matibabu pamoja na vifaa hafifu vya matibabu, bila kutaja magonjwa makubwa, hata upasuaji mdogo wa kawaida utaleta matatizo.

    Mjumbe wa kabila la Tatar wa mkutano wa Baraza la mashauriano la China Bw. Yiliduosi Ahetamofu alipokumbuka kifo cha babu yake, alisema:

    "wakati huo, hata upasuaji mdogo haukufanyika, kwa mfano ugonjwa wa kidole tumbo, babu yangu aliugua ugonjwa huo alipokuwa na umri wa miaka 55,kwa kuwa hawakuwepo madaktari wanaoweza kuutibu, babu yangu alifariki dunia. Huu kwa kweli ni upasuaji mdogo na rahisi. Nilipojifunza udaktari pia nilifanya upasuaji huo, lakini wakati huo mimi bado sijawa daktari rasmi."

    Hali hiyo ni mfano tu wa shughuli za utoaji huduma za afya za wakati huo katika sehemu za vijijini na sehemu ambazo zina waislamu wengi. Toka China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango kwa nje, hasa katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China imeweka mkazo katika utoaji huduma za afya kwenye sehemu za vijijini na kuimarisha ujenzi wa utaratibu wa utoaji huduma za matibabu vijijini, idadi ya hospitali kwenye sehemu za vijijini imeendelea kuongezeka, kiwango cha huduma za matibabu pia imeboreka kidhahiri, hali hiyo imekomesha jukumu la kihistoria kwa 'madaktari pekupeku' kutoa huduma za afya.

    Mjumbe Bw. Adalaiti alisema, katika miaka ya hivi karibuni serikali imenunua vifaa vingi vya kisasa vya matibabu kwa ajili ya hospitali za vijijini na hata zimeweza kufanya upimaji wa ultrasonic ya aina ya B na upimaji wa moyo, hali ya jumla ya matibabu imeboreka kidhahiri kuliko zamani.

    Bi. Guo Cunjun kutoka sehemu inayojiendesha ya Changxi ya mkoa wa Xinjiang anayefanya kazi mjini Beijing alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

    "Hivi sasa kwenye hospitali za vijijini, vifaa mbalimbali vya matibabu vyote vinapatikana, vikiwemo vifaa vya kujiandikisha, upimaji wa moyo, na upimaji wa CT."

    Imefahamika kuwa katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur ambao una waislamu wengi, takwimu za mwaka 2008 zimeonesha kuwa tangu China ianze kutekeleza utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano mwaka 2003, wilaya 89 za mkoa huo zote zimeshiriki kwenye utaratibu huo na watu milioni 10.05 wamenufaika, zaidi ya nusu yao ni waislamu. Utaratibu huo umehimiza maendeleo ya shughuli za huduma za matibabu vijijini za mkoa huo. Hivi sasa kila wilaya ina hospitali, kila kijiji kina zahanati, wafugaji na wakulima sasa wanaweza kupata huduma za matibabu kwa urahisi.

    Tarehe 5 mwezi Machi kwenye mkutano wa pili wa Bunge la 11 la umma la China, waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alipotoa ripoti ya kazi ya serikali aliweka hatua halisi za kukamilisha utaratibu wa kutoa huduma za matibabu vijijini. Alisema:

    "ya tatu ni kukamilisha utaratibu wa utoaji huduma za afya vijijini. Mwaka huu idara husika zinatakiwa kumaliza ujenzi wa vituo elfu 29 vya huduma za afya katika ngazi ya tarafa, kujenga hospitali katika wilaya 2000 na vituo 2400 vya huduma za afya mijini."

    Kuhusu hatua hizo alizoweka Bw. Wen Jiabao, mjumbe Yiliduosi alisema:

    "waziri mkuu Wen Jiabao alisema, China itawekeza yuan bilioni 850 kuhakikisha mageuzi ya utaratibu wa huduma za matibabu yanaendelea bila matatizo, mimi nikiwa ni mtumishi wa sekta ya afya, naamini kuwa chini ya uongozi wa rais Hu Jintao na waziri mkuu Bw. Wen Jiabao,\kazi ya utoaji huduma za afya kwa sisi waislamu itaendelea vizuri zaidi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako