• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Waafrika wapendelea mji wa Guangzhou

    (GMT+08:00) 2009-04-03 20:37:20

      

    Tukitaja mji mkubwa wa China, watu wengi wa Afrika watakumbuka zaidi kuwa siyo Beijing wala Shanghai, bali ni Guangzhou. Sababu yake ni kuwa, Guangzhou ni mji ulio karibu zaidi na bara la Afrika,na ni kituo cha kwanza nchini China ambacho watu wengi wa Afrika hufika, na pia ni chaguo la kwanza kwa waafrika kusoma na kufanya biashara.

    "Guangzhou ni mji unaovutia, sisi tuliposhuka kwenye ndege, sote tulishangaa sana, mji huo ni wa kuvutia mno, njia, nyumba, zote ni nzuri."

    Aliyesema hayo anaitwa Halima Hassan Nkuzi kutoka Tanzania. Alifika Guangzhou si zaidi ya mwezi mmoja, ambapo hii ni mara yake ya kwanza kuja China. Halima alihitimu masomo ya udakrari katika chuo kikuu cha Tanga, Tanzania, na baadaye alifanya kazi kwenye hospitali ya Mawenzi. Sasa Halima anasoma kwenye darasa la mafunzo ya ufundi wa kinga na tiba ya magonjwa ya tropiki kwa nchi za Afrika linaloandaliwa na chuo kikuu cha Udaktari cha kusini ambacho ni maarufu mjini Guangzhou. Mwanafunzi mwenzake wa chuoni nchini Tanzania Edith Minja Jacob alikuja hapa pamoja na Halima. Walimu wa darasa hilo wanawaitwa "kaka wawili wa Tanzania".

    "Kwa kweli hapa kuna tofauti kubwa na Tanzania. Mjini Guangzhou kuna majengo mengi makubwa, barabara ni nyingi, na aina za bidhaa ni nyingi sana. Tulitembelea hospitali ya hapa, na kujionea huduma kwa wagonjwa. Kufanya utafiti wa udaktari hapa ni rahisi zaidi kuliko kwetu, na zana za matibabu pia ni za kutosha zaidi."

    Sio tu wana kumbukumbu nzuri juu ya mji wa Guangzhou, "kaka hao wawili wa Tanzania" pia wanafurahia sana juu ya pande mbalimbali za chuoni. Kikiwa kituo kimoja kati ya vituo vya wizara ya elimu vya China vya kutoa misaada ya elimu kwa nje, chuo kikuu cha udaktari cha kusini siku zote kinafanya juhudi kutoa mazingira mazuri zaidi ya masomo na maisha kwa wanafunzi wa Afrika. Mabwalo matatu yenye aina tofauti za uzuri yalijengwa katika chuo hicho. Mkuu wa chuo hicho Bw. Zhaou Zenghuan alisema,

    "Tunaheshimu sana desturi za wanafunzi kutoka nchi mbalimbali, kama vile wakati wa sikukuu kubwa za kiafika, tunawandaa wanafunzi kufanya shughuli kadhaa. Zaidi ya hayo wakati wa likizo, tunawaandaa wanafunzi hao kutembelea sehemu fulani nchini China. Tuliwahi kwenda Beijing, Shanghai, Guilin, Jinggangshan, na miji mingine na sehemu nyengine zenye vivutio nchini China."

    Kusoma katika mazingira mazuri, wanafunzi wa Afrika wanaosoma nchini China wanasoma kwa furaha. Edith alisema, darasa hilo la mafunzo ya magonjwa ya tropiki kwa nchi za Afrika linawafundisha ufundi wa kinga na tiba ya magonjwa kadhaa ya maambukizi yanayoenezwa katika nchi za Afrika, kama vile ugonjwa wa ukimwi na malaria, walimu wanawafundisha kwa lugha ya kiingereza.

    "Masomo siyo magumu sana, ingawa masomo tunayosoma hapa tumeshasoma katika chuo kikuu nchini Tanzania, lakini hapa tunaweza kuimarisha elimu tunayopata, na pia kusoma mambo mapya, pia baadhi ya dawa hatukuwahi kuzijua kabla ya hapo."

    Kulingana na "kaka hao wawili wa Tanzania" ambao walikuja muda sio mrefu uliopita, Daniel Cago Wambugu kutoka Kenya tunaweza kumuita "mtu mwenye elimu nyingi kuhusu China". Sasa anasoma huku anafanya biashara ya samani katika soko moja mjini Guangzhou. Alipokutana naye kwa mara ya kwanza, mwandishi wetu alijifanya kuwa mteja, ili kujua kiwango chake cha lugha ya kichina.

    Mwandishi: Meza hiyo ni bei gani?

    Daniel: Ni yuan 1600.

    Mwandishi: Unaweza kupunguza bei kidogo?

    Daniel: 1500, basi.

    Mwandishi: 1000, sawa?

    Daniel: 1000? Haiwezekani.

    Mwandishi: Nipunguzie bei zaidi tafadhali.

    Daniel: Hapana, bei ya chini kabisa ni 1500.

    Ukisikiliza mazungumzo hayo, unaweza kufikiri kwamba mfanyabiashara huyo anayeongea lugha ya kichina vizuri na kwa mfululizo ni kijana kutoka Afrika?

    "Mimi naitwa Daniel Cago kutoka Kenya. Sasa nasoma lugha ya kichina katika chuo kikuu cha Shenzhen."

    Daniel ana historia nzuri ya elimu. Alihitimu masomo ya biashara ya kimataifa katika chuo kikuu cha Kenyata. Kutokana na shangazo kwa China, kijana huyo mwenye ndoto kubwa alikuja Guangzhou. Baada ya kufika hapa na kuingia chuoni, alitumia fursa zote kujifunza lugha ya kichina, hususan lugha ya mazungumzo, ili kujitahidi kujua vizuri maneno na sentensi nyingi zaidi ndani ya muda mfupi. Sasa ana imani kubwa juu ya kiwango chake cha lugha ya kichina, alisema,

    "Nafurahi sana kwamba sasa nasoma lugha ya Kichina, naweza kuwasiliana na wenzangu wa China na wenzangu kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lugha ya kichina. Tunazungumza kwa lugha moja, yaani lugha ya kichina."

    Kuwa na msingi mzuri wa lugha, pamoja na elimu yake ya biashara ya kimataifa, Daniel anaanza kufanya biashara kidogo kidogo akiwa nje ya darasa. Maisha hayo yanafurahisha Daniel, anajifunza mambo mengi nje ambayo hawezi kujifunza chuoni. Baada ya mwaka mmoja tangu aje China, Daniel ameshakwenda sehemu mbalimbali za kusini na kaskazini mwa China kwa ajili ya biashara, Beijing, Qingdao, Yiwu, Shanghai, n.k. miji yote hiyo ameshakwenda. Alijumisha uzoefu wake wa kufanya biashara, akieleza,

    " 'Yi Fen Qian, Yi Fen Huo' maani yake ni kwamba ukigharamika shilingi moja zaidi, sifa za bidhaa zitakuwa za kiwango cha juu zaidi. Najua sisi husema hivyo, 'Wo Xian Zai Kan Kan'. Wakati wa kufanya bishara baadhi ya maneno yana matumizi makubwa, kama vile kuuliza bei. Unaweza kusema, 'Zhe Ge Dong Xi Duo Shao Qian?' Na ukitaka kuuliza kama kuna bidhaa ambazo zimemalizika, unaweza kusema, 'Ni You Xian Huo Ma?' kama hutaki bidhaa zisizo na sifa bora, kwa sababu sifa za bidhaa zinazingatiwa sana nchini China, unaweza kusema hivyo, "Wo Yao Zhe Ge Zhi Liang, Qing Bie Huan Zhe Ge Zhi Liang."

    Kama ilivyo kwa Daniel ambapo bado anaburudika kwa kusoma lugha ya kichina, Chisulo Brian naye kutoka Zambia ameanza kupenda utamaduni mkubwa na wa kale wa China:

    "Nadhani jambo la kuvutia zaidi ni hisia yangu juu ya upande wa utamaduni, kama vile kula chakula. Ufundi wangu wa kula kwa kutumia vijiti ni mzuri sana."

    Kabla ya hapo, Chisulo alikaa mjini Shanghai kwa miaka mitano, na baada ya masomo alirudi Zambia kufanya kazi ya udaktari. Baadaye alikuwa na ndoto ya kuendelea na masomo, mwaka 2007 alirudi nchini China, na mara hii alichagua Guangzhou kuwa sehemu yake ya mwanzo ya kutimiza malengo yake makubwa. Mambo mengi ya kusoma na kuishi mjini Guangzhou yanamfurahisha:

    "Siku moja tulikwenda kwenye mkahawa mmoja, tulitaka kula samaki. Mhudumu alituletea samaki mmoja mrefu sana. Tulidhania ni nyoka wala siyo samaki, na kusema 'hatutaki huyo, hatutaki huyo, tunaogopa kula huyo'. Lakini mhuduma aliona vijana hao ni wa kushangaza, kwa kuwa samaki wa aina hiyo ni wa kawaida kwa watu wa China."

    Guangzhou, mji mzuri wa kusini mwa China, unakaribisha sana kila mgeni kutoka Afrika na sehemu mbalimbali duniani. Tuna imani kuwa kila mmoja aliyefika hapa atakuwa kumbukumbu nzuri. Labda maneno hayo ya dhati ya Chisulo yanaweza kueleza maoni ya watu wengi:

    "Nitakuwa na kumbukumbu nzuri zaidi katika maisha yangu kwa siku nilizokaa nchini China. Nimetembelea nchi nyingi, lakini maisha ya hapa China ni ya pekee, ninafurahi sana. Kuja hapa sitajuta kamwe, na huu utakuwa uzeofu mzuri zaidi katika maisha yangu."

    Waafrika wengi wanaoishi Guangzhou wanachukulia hapa kuwa ni nyumba zao nyingine, na wanajisikia na kujiburudisha kwa furaha kila siku za hapa .

    Wasikilizaji wapendwa, katika vipindi vinavyofuata, tutakuleteeni hadithi nyingi zaidi juu ya wanafunzi wa Afrika wanaosoma nchini China.. Asanteni kwa kutusikiliza, kwa herini!

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako